NA ABDI SULEIMAN

MBUNGE wa Jimbo la Kojani Wilaya ya Wete, amewataka wasimamizi wa mpango shirikishi wa shehia ya Kiuyu Kigogoni kuhakikisha wanaunda kamati ya ufuatiliaji na Tathmini, ili kuona kilichopangwa kinafanyika kwa wakati muwafaka.

Alisema kamati hiyo itaweza kuwakumbusha viongozi wanaosimamia mpango kuwa, kama kutakua na vipaombele havijatekelezwa na vilipangwa kufanyika.

Hayo aliyaeleza wakati wakikao cha uwasilishaji wa Vipaombele vya mpango shirikishi wa shehia hiyo, mkutano uliofanyika Kiuyu Kigongoni Wilaya ya Wete.

Alisema vipaombele vilivyoibuliwa vya afya, kilimo na elimu ni vipaombele muhimu sana kwa shehia hiyo, hivyo kamati hiyo inapaswa kuhakikisha vinatekelezwa kwa wakati kwa kushirikiana na taasisi husika.

“Hongereni sana taasisi ya Milele Zanzibar Foundation katika juhudi zenu zakusaidia serikali na wananchi wake, huu mpangao umewaonyesha wananchi changamoto zao kubwa zinazowakabilia kama afya, elimu na kilimo”alisema.

Aidha, aliwashauri walimu wa skuli ya Kiuyu kuhakikisha wanaunda kamati maalumu ambayo, itaweza kusimamia suala la ufundishaji skulini hapo, kwa kutafuta wanafunzi waliomaliza vyuo na wanauwezo mkubwa wa kusaidia ndugu zao kwenye elimu, ili kurudisha hadhi ya ufaulu kwa asilimia 60%.

Hata hivyo, Mbunge huyo alisikitishwa na tabia ya madaktari katika kituo cha afya kiuyu Minungwini, kuondoka kazini wakati muda wakazi bado hali inayowapatabu wagonjwa waofuata matibabu kituoni hapo.

“Mimi binafsi nilifika kituoni na kukuta wagonjwa wapo ila daktari hayupo, muhudumu aliwawataka warudi siku nyengine ikizingatiwa muda wa kazi upo, nikajuwa tatizo sio uhaba wa madaktari bali ni madakatri wenye wanashindwa kuwajibika”alisema.

Mbunge huyo aliwataka wataalamu wakilimo kuhakikisha wanashuka kwa wananchi vijijini, kwa lengo la kuwapatia taaluma bora wakulima ili kulima kibiashara na kuondokana na kulima kimazowea.

Mratib wa miradi ya afya kutoka Milele Zanzibar Foundation Shemsa Nassor, alisema wananchi wanajibu wa kufuatilia mpango shirikishi kwa ajili ya kujuwa maendeleo ya shehia yao.

“Niwajibu wenu wananchi kufuatilia pamoja na kutoa mashirikiano katika kamati hii ya mpango shirikishi, ili muweze kuona nini kilichofanywa na viongozi katika shehia yenu”alisema.

Naye diwani wa wadi ya Kiuyu Nasra Salum Moh’d, alisema serikali inaimani sana na wananchi wake ndio ikataka wananchi kuibua changamoto zao kwenda serikali kuu.

Hata hivyo wananchi wa shehia ya kiuyu kigongoni Wilaya ya Wete, wamesema kuwa changamoto kubwa zinazowakabili katika shehia yao ni Kilimo, afya, Elimu na barabara.