Mchango wa Kihindi katika lugha ya Kiswahili
Na Mohamed Mzee Ali(Tere), SUZA
Lugha ya Kiswahili pamoja na kutolewa nadharia kadhaa kuhusu lugha hiyo kama Kiswahili ni Kiarabu, Kiswahili ni Kibantu na Kiswahili hakina mwenyewe bali ni lugha ya watu wote, lakini ukweli unabaki kuwa Kiswahili ni lugha nzuri yenye kujitegemea kwa kila kitu.
Hata hivyo, kama zilivyo lugha nyengine duniani, Kiswahili kinakua na kupata baadhi ya msamiati kutoka lugha nyengine kadhaa za dunia. Miongoni mwa msamiati uliomo katika Kiswahili kutoka lugha nyengine ni ule wa lugha ya Kihindi.
Kwa mujibu wa historia, msamiati wa Kihindi katika lugha ya Kiswahili uliingia baada ya kuja Wahindi wengi Zanzibar kwa biashara na hatimaye kufanya mastakimu yao hapa.
Sultan wa mwanzo wa Zanzibar Seyyid Said Bin Sultan alipofanya makaazi yake ya kudumu hapa Zanzibar badala ya Oman mnamo mwaka 1832, alimuajiri Muhindi mmoja maarufu aliyeitwa Taaria Topan kuwa Mkusanyaji Mkuu wa Kodi katika biashara zinazofanyika hapa Zanzibar.
Kufuatia kuja kwa Muhindi huyo, wahindi wengine walianza kuingia kwa wingi kwa madhumuni ya biashara za aina mbali mbali na kisha kufanya mastakimu yao hapa Zanzibar hasa katika eneo la Shangani katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Katika muamala wa kibiashara wahindi wakiwa na lugha yao, msamiati wao mwingi ilibidi kuingia katika Kiswahili ili biashara iendelee vizuri na kujenga mafahamiano na Waswahili waliokuwepo wakati huo.Lugha hizo za kihindi ni pamoja na Urdu, Gujirati, Hindi nk.
Mara nyingi biashara huendeshwa kwa sarafu na ikasadifu kuwa kwa vile Zanzibar ni kitovu cha biashara, sarafu mbali mbali zikaanza kutumika. Mathalan, wahindi walikuja na Rupia ambayo ni sarafu ya India na kutumika pia Zanzibar.
Sarafu ya Rupia iliingia katika lugha ya Kiswahili na ndio maana ukaja msemo “Penye Udhia penyeza Rupia” yaani udhia na matatizo hutatuliwa zaidi kwa njia ya pesa.
Neno Pesa nalo pia lina asili ya Kihindi kwa hapa kwetu Zanzibar.Mara nyingi Wahindi walikkuwa wakisikika wakisema “Peisa Nehi .Chakatarega?” . Maana ya kauli hiyo ni kwamba” Sina pesa . Nifanye nini?”. Kwa maana hiyo Wahindi ndio walioliingiza neno hilo katika Kiswahili.
Wakati biashara Zanzibar wakati huo imeshika kasi, bandari ya Zanzibar ilijipatia umaarufu mkubwa na kuwa kituo kikubwa cha biashara Afrika Mashariki.
Bidhaa mbali mbali ziliiingia na nyengine kutoka kama vile karafuu, mbata , pilipili hoho na viungo, ambapo kuliibuka ajira ya watu kubeba mizigo bandarini hapo.
Wahindi walikuwa wanawaita wabeba mizigo hiyo hapo bandarini kwa jina la Khuli na hapo ndio jina Kuli kwa maana ya wabeba mizigo bandari likaanza kutumiwa.
Neno hili Kuli limesadifu kuwa na maana sawa na maneno kama mpangazi, mchukuzi na hamala.
Aidha, bila shaka katika biashara fedha ni lazima ihesabiwe.Wakati huo ilikuwa si sana watu kuhesabu kufikia milioni, bilioni na kadhalika kama ilivyo sasa. Fedha nyingi ilikuwa katika Mamia na Laki.
Kwa bahati Wahindi walihesabu hadi kufikia Lakh . Sasa neno hili likaingia katika muamla wa fedha na kubakia katika Kiswahili Laki yaani 100,000. Kiingereza hakuna neno Laki.
Vyombo vya usafiri navyo viliingia Zanzibar na miongoni mwa hivyo ni magari. Gari zilizokuwa maarufu ni hizi ndogo ambazo kwa Kiingereza zilifahamika kwa car au motor car.
Waswahili waliviita vyombo hivi vya usafiri kwa jina la ‘Mutukari’ au ‘motokaa’. Hata hivyo, maneno haya hayakushika kasi sana labda kutokana na kutamka kwake kuwa kugumu kidogo na kutumika zaidi “car”.
Kwa vile wahindi mara nyingi hawatamki Kiingereza sawasawa, bali hutawaliwa zaidi na matamshi ya Kihindi , neno ‘car’ wakawa wanatamka ‘gar’. Kwa maana hiyo neno hili likashika kasi na kuwa ‘gari’.
Waswahili wana msemo usemao “ usinifanye punda wa dobi”. Msemo huu una maana kwamba usimbebeshe mzigo mkubwa ukadhani kuwa ni mwepesi wakati ni mzito.
Msemo huu unatokana na kwamba zamani walipokuja Wahindi kulikuwa na watu waliokuwa kazi yao kufua nguo kwa kibarua na kupiga pasi. Kazi hii ilianzishwa na Wahindi wale ambao kipato chao ni cha chini.
Wahindi hao walijulikana kwa jina la ‘DOBI’ na walikuwa wanawatumia punda kubeba nguo nyingi na kupeleka sehemu za mafulio kwa kufuliwa. Hivyo, neno ‘Dobi’ linatokana na Kihindi.
Itakumbukwa kuwa vazi la Kanga lilianzishwa na Wahindi na ndio waliokuwa wachapishaji wakubwa wa vazi hilo. Ukisikiliza hotuba ya Marehemu Mzee Karume alisema ‘kuanzia Mlandege hadi kwa Hajitumbo kote kulikuwa kunauzwa kanga’.
Wakati huo na hadi leo kanga ilikuwa inauzwa kwa pande mbili na wahindi waliita ‘Dhoti’. Neno hili lilitumika na kushika kasi na kutumika hadi leo kama “Doti”. Na ndio maana watu husema nipe doti moja ya kanga.
Aidha ,katika Kiswahili kuna kivumishi “ Bora”. Neno hili nimeliangalia sana na halimo katika lugha za Kibantu wala Kiarabu. Nilipotafiti zaidi nikagundua la Kihindi kwa kuwa neno ‘Bora’ linatokana na lugha ya Kihindi na kusadifu kulisikia katika filamu za Kihindi.
Kadhalika nimesadikisha kuwa neno hilo ni la kihindi kwa kuwa niliwahi kufanyakazi na Muhindi mmoja wa Kampuni ya Transpapers ya Dar es Salaam nilipokuwa Wakala wa Uchapaji Zanzibar akiitwa Mr. Bora.
Kama nilivyotangulia kusema kuwa Wahindi walikuwa ni wafanyabiashara wakubwa wakati huo. Waliingia katika kila biashara hata kuku wa kinyeji. Ilisadifu siku moja mtu mmoja kutoka Bambi alimuuzia Muhindi kuku kumbe ndani yake mna matipitipi wengi kuliko kuku wa kienyeji.
Baada ya muda kupita ulipofika muda wao watipitipi yakalia na muhindi kusema “ mshamba jinga sana”.
Wahindi pia kwa wakati huo ndio waliokuwa wafanyabiashara wakubwa wa dhahabu na fedha. Kwa lugha ya Kihindi wafanyabiashara hiyo walijulikana kwa jina la“Sonara” . Jina hilo moja kwa moja likaingia katika Kiswahili hadi leo.
Kadhalika, wahindi pia walikuja na biashara ya kudhamini vitu kama nyumba , mashamba na kadhalika huku anaedhaminiwa akilipa ada fulani kwa muda maalum. Biashara hii ilijulikana kwa jina la “Bhima”.
Neno hili “Bhima” liliingia katika lugha ya Kiswahili ambalo hivi sasa ndio “Bima”, ambayo hukatiwa biashara, vyombo vya moto na kadhalika.
Hivi sasa watu wengi utawasikia fulani kaandikiwa Cheki ya shilingi 500,000. Neno ‘Cheki’ ni la Kiingereza ‘Cheque’, ambayo ni karatasi maalum inayoandikwa kiasi cha fedha kumlipa mtu kwa kuivunja benki.
Ukweli neno hili si la Kiswahili, bali neno lililokuwa linatumika asili ni ‘Hundi’. Neno hili asili yake ni lugha ya Kihindi na likaingia katika muamala wa kifedha katika lugha ya Kiswahili.
Zamani wakati Wahindi wameshika kila aina ya biashara, kulikuwa na biashara ya kuuza nguo kuukuu pia. Biashara hii ilijulikana kwa jina la “Poni”. Neno hili lilitumika sana, lakini hivi sasa biashara hiyo inajulikana kwa jina “ mitumba”.
Ukweli ni kwamba lugha ya Kihindi imeliingiza neno hilo ‘poni’ katika msamiati wa Kiswahili ingawa siku hizi limepuuzwa.
Katika Kiswahili watu wanaofanya hujuma ya kuwaua wanyama katika hifadhi wanajulikana kama ‘majangili’. Neno hili ‘jangili’ halina asili ya lugha za kibantu wala Kiarabu kama ambavyo maneno mengi yanafahamika etimolojia yake. Hivyo, neno hili asili yake ni Kihindi na utalisikia sana katika Senema za Kihindi.
Mtu anaenyang’anya mali za watu kwa nguvu na hata kutumia silaha hujulikana kwa jina la ‘jambazi’. Neno hili nalo asili yake ni Kihindi na limeingia katika msamiati wa Kiswahili baada ya Wahindi kuishi hapa Unguja kwa miaka kadhaa. Hata hivyo, neno ‘chori’ kwa maana ya mwizi nalo hutumika ingawa si sana.
Kwa kawaida Waswahili wana tabia ya kutandika pahala pa kulala. Pahala hapo hutandikwa kwa kifaa kinachoitwa ‘tandiko’. Hapo zamani tandiko hutengenezwa kwa usufi na usumba.
Kadiri siku zinavyokwenda na mambo hubadilika. Yamekuja matandiko ya kisasa yanayojulikana kwa jina la’ magodoro’.
Neno ‘godoro’ halina asili ya Kiswahili, bali ni msamiati unaotokana na Kihindi na kwa muktadha huo ‘godoro’ limechukuliwa kuingizwa katika Kiswahili kutoka lugha ya Kihindi.
Kuna Waswahili wengine hadi leo wanatumia neno ‘furniture’ wanapotaka vifaa vya nyumbani vinavyotengenezwa kwa mbao kama kitanda, kiti , meza, makochi nk.
’Samani’ kwa maana ya vifaa vilivyotajwa awali, pamoja na kutumika neno hilo, lakini halitokani na lugha za kibantu, bali asili yake hasa ni Kihindi na hasa katika lugha ya ‘Urdu” inayozungumzwa zaidi Pakistan na Bangladesh.
Neno hili limeingia katika msamiati wa Kiswahili kutoka lugha hiyo walipokuja wahindi.
Siku hizi utawasikia watu hasa wanawake na wapambaji harusi kuwa tunataka ‘shela’ ya kuburura katika nguo ya harusi. Harusi za Kiswahili hazikuwa na nguo za aina hiyo, bali zilitosha kanga za kisutu.
Hili neno ‘shela’ kwa maana ya kipande cha juu kinachokuwa kichwani katika nguo za siku hizi za harusi, limeingia katika msamiati wa Kiswahili kutoka Lugha ya Kihindi.
Zamani manukato au uturi ulikuwa unapimwa vipimo maalum kabla ya hivi sasa kuwemo katika chupa ndogo ndogo na za kupuliza. Vipimo hivyo vilijulikana kwa jina la “Tola”. Akinamama walipimiwa katika vichupa vyao walivyokuwa wakiwasilisha muuzaji.
Hili neno ‘Dukani” lililomo katika lugha ya Kiswahili, nimelikuta katika lugha kadhaa. Neno hili ukiangalia katika lugha ya Kiarabu unalikuta halkadhalika katika Kihindi kwa jina la’ Dukan’. Kwa muktadha huo neno hili ‘dukani’ linatokana na lugha hizo mbili.
Sambamba na hilo neno “Dunia” ambalo limo ndani ya Kiswahili pia linapatikana katika Kihindi’Dun’ya’ na pia Kiarabu. Sasa nani mwenyewe neno hili linahitaji utafiti, lakini takriban lugha zote duniani zinategemeana.
Katika mapishi huko ndio usiseme. Kiswahili kimepata msamiati mwingi sana kutoka lugha ya Kihindi. Msamiati huo ni pamoja na Biriyani, Pilau(pullao), ladu (ladoo), bajia, kachori, achari, chapati(mkate wa kusukuma) nk.
Pia katika Kiswahili kuna neno ‘pwani”. Neno hili kuna wasiwasi mkubwa huenda likawa linatokana na lugha ya Kihindi. Ninasema hivyo kwa kuwa katika lugha ya Kihindi maji yanaitwa ‘pani’.
Kwa muktadha huo inawezekana neno pwani ambako kuna maji mengi ya bahari wakaona waite ‘pwani’ kutoka neno ‘pani’ lenye maana ya maji kwa Kihindi. Hata hivyo, utafiti zaidi wa etimolojia ya neno unahitajika.