Yajue maneno ya Kiswahili yenye utatanishi

NA MWANDISHI WETU

KATIKA lugha ya Kiswahili kuna baadhi ya maneno yanayoleta utatanishi kwa watumiaji kutokana na sababu mbalimbali. Baadhi ya sababu zinazochangia utatanishi huo ni pamoja  na kutumia neno lisilo sahihi badala ya lile sahihi, kutojua maana halisi ya neno analotumia mzungumzaji, kuchanganya maana ya maneno mawili yenye maana tofauti au pengine kuiga matumizi yasiyo sahihi ya neno au maneno fulani kutoka kwa baadhi ya watu. Vilevile tatizo hili linachangiwa na kushindwa kwa mtumiaji kutamka kwa usahihi neno fulani.

Katika makala haya tutazungumzia baadhi ya jozi za maneno ya Kiswahili ambayo watumiaji tumekuwa tukiyatumia kimakosa au kuchanganya maana. Baadhi ya maneno hayo ni  Chonota na Chonyota, Panua na tanua, Guna na guta, Pahala, Pahali, Mahala na Mahali, Pumua na hema, Kajeli na Kebehi na maneno mengineyo.

Chonota na chonyota ni neno lenye maana moja ambapo  maneno hayo mawili maana yake ni hali ya kuwashawasha katika sehemu fulani za mwili hasa zenye jeraha au kidonda. Kama mtu ana kidonda na pengine kidonda au jeraha hilo likaingia kitu chenye kusababisha uwasho kama vile maji ya pwani au dawa yenye kuwasha basi hali hiyo ni kuchonyota au kuchonota.

Vilevile unapokuwa na jeraha au kidonda katika ulimi na ukila kitu chenye ladha ya ukali kama vile embe mbichi au mchuzi ulochapuka, hali hiyo husababisha kuchonyota au kuchonota kwa ulimi.

Chanua, panua na tanua ni maneno yenye maana tofauti. Chanua ni kitendo cha ua la mti au mmea kufumbua. Vilevile neno hilo maana yake nyengine ni kupanua nafasi ambayo ilikuwa imebana. Tanua maana yake ni kitendo cha kuvuta  eneo, wigo au sehemu ili kuongeza nafasi. Mfano unapoongeza eneo la shamba lako maana yake umetanua shamba hilo. Panua ni kuongeza upana au eneo la nafasi. Mfano, uwanja wa ndege wa Zanzibar unapanuliwa.

Guta na guna ni maneno tofauti ambapo katika Kiswahili neno guta lina maana mbili. Maana ya kwanza ya neno “Guta” ni kitendo cha kutoa sauti ya maumivu au kejeli. Mara nyingi mtu fulani anaposema neno, kutoa kauli au kufanya jambo ambalo unalidharau unatoa sauti ya kuguta kuonyesha dharau au kejeli kwa mtu huyo. Kosa kubwa ambalo wengi tunalifanya ni kutumia neno, “ugua” kwa maana ya “guta” pale mtu anapotoa sauti ya maumivu anapokuwa kitandani anaumwa au anapopata ajali. Guna au kuguna ni kutoa sauti ya ndanindani  au chini chini yenye kuonesha kutoridhishwa na jambo au kitendo fulani.

Kwa mfano kama bosi wako kazini ametoa amri kwamba lazima siku ya Jumapili ambayo ni siku ya mapumziko mfike kazini, kutokana na kutoridhika na maelekezo hayo “Unaguna” kwa vile hilo jambo hulitaki lakini huna la kufanya.

Kejeli  na kebehi ni maneno yenye maana moja ambapo maneno haya yana maana mbili tofauti. Maana ya kwanza ya kejeli au kebehi  ni matamshi, neno, kauli au tendo lenye kuashiria dharau kwa mtu. Maana ya pili ya maneno hayo ni kitendo cha kumwambia mtu neno au kumfanyia tendo lenye kuonesha dharau. Vilevile kejeli na kebehi maana yake ni kitendo cha kutoa hadhi au kudhalilisha kitu, mtu au jambo fulani.

Mahali, Mahala, Pahali na Pahala ni  neno lenye maana moja, lakini tunafanya makosa ya kimatamshi. Neno sahihi la Kiswahili kati ya maneno manne hayo ni “Pahala” ambapo maana yake ni  eneo au nafasi alipo mtu au kitu. Mfano,  “Ali yuko   darasani”. Neno “darasani” ni pahala alipo  Ali. Lakini pia tunatumia neno, “mahali” kwa maana hiyo. Maneno “mahali” na “mahala” pia yanatumika lakini sio rasmi kwa lugha fasaha.

Maneno mengine yenye kutuchanganya kimatumizi ni Mapele, Upele na Vipele. Neno sahihi la Kiswahili ni “Upele” ambalo maana yake ni vivimbe au vijeraha vidogo vidogo vyenye kuwasha na kutoa maji maji vilivyoshikamana katika ngozi. Kosa kubwa  tunalofanya ni Upele kuuita Vipele, labda hali hiyo inatokana na udogo wa vijeraha hivyo.

Koroma, Nguruma, Vuma na Korota ni maneno tofauti ambayo  yanatupa shida katika matumizi. Katika Kiswahili neno “koroma” lina maana tatu. Maana ya kwanza ni nazi ambayo haijapea vizuri.

Maana ya pili ni nazi changa inayopatikana mara tu baada ya kuzaliwa ambayo pia inaitwa Kokochi. Maana ya tatu ya neno “Koroma” ni kitendo cha kutoa sauti kubwa ya pumzi wakati mtu anapolala. Korota ni neno linalotumiwa na baadhi ya watu kumaanisha kukoroma, lakini neno hilo ni kilahaja cha baadhi ya sehemu za Zanzibar na sio rasmi. Nguruma ni kutoa sauti nzito yenye nguvu na iliyochanganyika.

Mara nyingi  sauti ya kunguruma hutokana na mashine kama vile ya meli, gari, ndege au jenereta. Vilevile  wanyama  kama Simba, Chui na Kifaru hutoa sauti ya kunguruma. Vuma ni neno lenye maana mbili ambapo maana ya kwanza ni kitendo cha kuwa maarufu au kutajwa sana.  Maana ya pili ni sauti inayotokana na upepo au wadudu kama vile nyuki wakiwa katika mwendo.

Churura na churuza ni maneno yenye maana moja ambayo ni hali au kitendo cha kutiririka kitu cha majimaji.

Telea na Teleza  ni maneno yenye maana tofauti. Katika Kiswahili neno “Teleza” lina maana tatu tofauti ambazo ni kwanza hali ya kitu kuwa laini sana kiasi cha kukifanya kitu chengine kutelea.

Mfano, Tope ni laini na hivyo zinateleza na kumfanya mtu anayepita atelee. Kwa lugha nyengine tope zinafanya “Utelezi”. Maana ya pili ya neno “teleza” ni kufanya kosa dogo kwa bahati mbaya. Pengine kosa hilo ni la matamshi, ndio maana tunasema, “ulimi umeteleza”. Maana ya tatu ya neno “teleza” ni kuserereka. Tofauti na neno hilo, neno “telea” maana yake ni kitendo cha kutaka kuanguka.

Tizama na tazama ni neno lenye maana sawa ambalo lina  maana mbili katika Kiswahili. Maana ya kwanza ni kumuhudumia mtu kwa kumpatia mahitaji yake ya lazima kama vile nguo, chakula na makaazi (kimu). Maana ya pili ya tizama au tazama ni kitendo cha kukodolea macho mtu, jambo au kitu kwa makusudi kwa lengo la kuona kile kinachofanyika.

Unyevu, Ukungu, Mvuke na Umande ni maneno mbalimbali yenye maana tofauti. Unyevu ni umajimaji ulioko kwenye kitu ambacho kimewekwa kwa muda mrefu katika sehemu ambayo haipati mwangaza wa jua. Mfano matofali yaliyowekwa kiwambazani pasina kupata mwangaza wa jua hufanya unyevu sehemu ya chini.

Ukungu ni neno lenye maana mbili, maana ya kwanza ni wingu jepesi la mvuke linalotanda juu ya ardhi au hewani na kusababisha giza. Mara nyingi ukungu hutanda wakati wa asubuhi hasa sehemu zenye milima yenye ubaridi au uwanda. Maana ya pili ni weusi wenye nyuzinyuzi unaofanya juu ya kitu kilichovunda.

Mfano mkate wa boflo ambao umewekwa katika kabati kwa muda wa wiki mbili bila kuliwa hufanya ukungu. Mvuke ni ukungu unaotokana na maji yanayochemka au yaliyopata joto (muye). Umande ni unyevunyevu unaotanda katika majani wakati wa alfajiri kutokana na baridi.

Funika, Fumba, Funga ni maneno yenye maana tofauti ambapo neno “Funika” maana yake ni kitendo cha kuzuia kuonekana kitu fulani kwa kuweka kuweka kitu chengine juu yake. Mfano tunatumia kawa kufunika chakula.

Hapa ifahamike kuwa pia kuna neno “kizibo” ambacho kinatumiwa kuziba chupa au mkebe kwa lengo la kuzia kile kilicho ndani ya chupa hiyo kisimwagike. Neno “fumba” lina maana tano tofauti ambapo maana ya kwanza ni unyayo wa mnyama kama vile Chui au Simba ambao huonekana pale anapofucha kucha zake.

Maana ya pili ya neno “fumba” ni mkake uliokwishashonwa ambao haujapasuliwa na kuwa katika umbo linalowezesha kutumika. Maana ya tatu ni pakacha ndefu nyembamba.

Maana ya nne ni kitendo cha kukutanisha pande za kitu zilizoachana. Mfano tunapofumba jicho tunakutanisha pande mbili za jicho hilo ambazo ziliachana kwa kuwa wazi. Maana ya tano ya neno “fumba” ni kutumia lugha ya mafumbo kumsema mtu au jambo fulani.

Neno “funga” kwa upande wake  lina maana tatu tofauti ambazo kimaana hazifanani na maneno funika na fumba. Maana ya kwanza  ya neno “funga” ni kufunga saumu katika mwezi wa ramadhani. Maana ya pili ya neno hilo ni kitendo cha kushikiza kitu kwa kutumia kamba, mnyororo au kufuli. Maana ya tatu ni hali ya kushinda katika mchezo kwa kufunga magoli mengi au kupata alama nyingi katika mchezo huo.

Baa na balaa ni maneno yenye maana moja ambayo ni janga lililoikumba jamii au kumpata mtu binafsi. Ingawa maneno, “baa na balaa” yana maana hiyo, lakini neno “baa” peke yake lina maana nyengine ambazo ni tofauti na balaa. Maana ya kwanza ya neno “baa” ni pahala panapouzwa na kunywewa ulevi hapo hapo. Maana nyengine ya “baa” ni mtu muovu.

Maneno mengine ambayo yanatupa shida katika matumizi ni Penda, Taka na Tamani. Haya ni maneno yenye maana tofauti ambapo neno “penda” maana yake ni hali ya kuvutiwa na mtu, kitu au jambo kutokana na uzuri au ubora wake.

Vilevile kupenda maana yake ni kuamua kufanya jambo au kitu fulani kutokana na  kuridhika nalo. Neno “tamani” lina maana mbili ambazo ni tabia ya kuwa na hamu ya kila kitu.

Maana ya pili ni kitendo cha kuwa na hamu au haja ya kupata kitu. Hapa ifahamike kuwa maana ya pili ya neno “tamani” tuliyoeleza ni hali ya kutamani kitu kwa kipindi fulani. Mfano mtu ameamka asubuhi na siku hiyo anatamani supu ya pweza. Lakini kesho yake akiamka asubuhi anatamani chapati na samaki wa kukaanga.

Maana ya kwanza ya neno “tamani” ni tabia ya kuendelea ya kutamani vitu mbalimbali ambapo mtu mwenye tabia hiyo huitwa “Mtamanifu”. Neno “taka” lina maana tatu  ambazo ni kitu au vitu vinavyosababisha mahala fulani pawe pachafu  yaani uchafu. Maana ya pili ni kuhitaji jambo au kitu. Maana ya tatu ni kitendo cha kuwa katika hali ya kufanyika au kutokea muda mfupi ujao.

Nyonya na fyonza ni maneno mawili  mbalimbali yenye maana tofauti. Nyonya maana yake ni kitendo cha kuvuta kwa ndani kitu cha majimaji kwa kutumia mdomo, mrija au mashine yenye kufanya hivyo. Vyoo au mashimo ya karo yaliyojaa maji machafu husafishwa kwa kutumia gari maalum yenye kunyonya uchafu huo.

 Fyonza ni kitendo cha kuvuta au kufuta kitu cha majimaji kwa kutumia kitu kama kitambaa, spanji, ulimi au mrija kama anaotumia nyuki kufyonza asali katika maua. Mshangao, Butwaa na Bumbuazi ni maneno yenye maana moja ambayo ni hali ya mtu kutulia, kuemewa na kukaa kimya kwa muda bila ya kufanya kitu chochote au kujua nini cha kufanya.

Kugudi, Kusugudi, Kisigino  haya ni maneno matatu ambayo yana maana mbili tofauti. Kusugudi na Kigudi ni neno lenye maana moja ambayo ni kiungo kwenye mkono kinachounganisha mfupa mrefu unaoishia katika kiganja na mfupa mfupi unaoishia begani. Kisigino ni sehemu ya nyuma ya unyayo.  Kiza na giza ni maneno yenye maana moja ambayo ni hali ya kutokuwepo au kukosekana mwangaza.

Gamba na ganda  ni maneno mawili yenye maana tofauti. Katika  kiswahili, neno ganda lina maana nne tofauti. Maana ya kwanza ni sehemu ya nje ya tunda, mzizi au gome linalozunguuka kigogo cha mti.

Vilevile maana hiyo inaweza kutumika kumaanisha mashuke ya nafaka kama vile mpunga, mtama au uwele.  Maana ya pili ya neno hilo ni hali ya kukwama au kuzuilika bila ya kuwa na uwezo wa kwenda upande wowote.

Mfano gari imeganda mtoni. Maana ya tatu ya neno “ganda” ni  hali ya kitu kugeuka kutoka hali ya umaji maji na kuwa kigumu. Mfano lami imeganda barabarani. Maana ya nne ya neno hilo ni hali ya kitu kunata, kama vile linavyonata gundi.

Gamba ni neno lenye maana tofauti na ganda ambapo katika Kiswahili, neno gamba lina maana mbili tofauti. Maana ya kwanza ni kipande kigumu mithili ya palastiki kinachoganda katika mwili wa samaki, mamba, guruguru au nyoka. Vilevile kobe na kasa wana gamba gumu ambalo ndio sehemu ya mgongo wa viumbe hao. Maana ya pili ya neno, “gamba” ni karatasi ngumu inayotiwa sehemu ya nje ya buku la kuandikia au kitabu.