Dk. Mwinyi ataka tathmini majengo Mjimkongwe
NA KHAMISUU ABDALLAH
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wadau wa Mji Mkongwe ikiwemo Mamlaka ya Mji huo, Kamisheni ya Wakfu na Shirika la Nyumba Zanzibar kufanya tathmini ya ubora wa majengo yaliyopo Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Alisema majengo ambayo yapo katika hali mbaya haraka yafungwe na tathmini hiyo ielekeze katika kuhakikisha majengo hayo yanafanyiwa matengenezo ya haraka ili yasilete madhara.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kuwatembelea majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Mnazimmoja kuzifariji familia zilizoondokewa na jamaa zao wawili kutokana na ajali iliyotokea juzi ya kuporomoka sehemu za jengo la Beit- al- Ajaib.

Alisema hakuna sababu kuona nyumba ambazo zipo katika hali mbaya ziendelee kukaliwa, hivyo ni wajibu wao kufanya tathimini ya haraka ili serikali iweze kuchukua hatua ikiwemo kuzifanyia ukarabati.

Dk. Mwinyi pia alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na kuchukua hatua madhubuti ili kudhibiti maafa mengine kutokea.

Hata hivyo, aliwapongeza madaktari wa hospitali hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuwahudumia majeruhi wa ajali hiyo ambao ni mafundi waliokuwa wakilifanyia ukarabati jengo hilo la kihistoria.

Akizungumzia changamoto alizopata kwa wagonjwa wengine ikiwemo wodi ya kisukari na wodi ya waliovunjika, alisema ni kweli kuna upungufu wa vifaa na tayari ameshatoa maelekezo kupatikana kwa vifaa hivyo.

Aliwaomba ndugu walioondokewa na jamaa zao kuwa na subira katika kipindi kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao kwani msiba huo sio wa familia pekee bali ni wa Taifa kwa ujumla na serikali itachukua gharama zote za mazishi.

Aidha aliwapa pole majeruhi wanne wanaoendelea na matibabu katika hospitali ya Mnazimmoja na kupata majeraha mbali mbali katika miili yao na kuwaombea kwa Mwenyezimungu kupona haraka ili kuendelea na ujenzi wa taifa, huku serikali ikiwa pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.

Sambamba na hayo Dk. Mwinyi aliwashukuru wananchi kwa kushirikiana na serikali katika kusaidiana katika ajali hiyo na kutoa salamu zao za pole na kuahidi kwamba wataendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo yanadhibitiwa.

MAALIM SEIF ATEMBELEA WAGONJWA
Katika hatua nyengine Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alipata fursa ya kuwatembelea majeruhi waliolazwa hospitali ya Mnazimmoja kwa lengo la kuwajulia hali sambamba na kuwapa mkono wa pole.

Aidha Maalim Seif pia alipata nafasi ya kutembelea katika eneo lilipotokea tukio la kuporomoka kwa jumla la Beit- al- Ajaib.

Akiwa katika eneo hilo, Maalim Seif aliutaka uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kushirikiana na Mamlaka ya Mji Mkongwe kufanya tathmini ya majengo yote yaliyokuwepo katika Mji mkongwe wa Zanzibar ili kunusuru maisha ya watu wengine.

Alisema, majengo mengi ya Mji Mkongwe ni ya zamani na yapo katika hali mbaya kutokana na ubora wake na tofauti na majengo ya sasa kutokana na muda mrefu hayajakarabatiwa.

Maalim Seif aliwapongeza Askari wa Vikosi vya SMZ, Jeshi la Polisi na JWTZ kwa kufanya kazi ya mfano ya kujitolea toka kutokea kwa ajali hiyo na kufanikiwa kuwaokoa majeruhi wanne ambao wanaendelea na matibabu katika hospitali kuu ya Rufaa ya Mnazimmoja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kuwataja waliofariki kuwa ni Pande Haji Makame (39) ambaye mkaazi wa Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja ambae alipatikana majira ya saa 6:00 usiku akiwa na majeraha ya kukatika vipande viwili.

Alisema mwili mwengine wa marehemu Buruhan Ameir Mavuno (25) mkaazi wa Daraja bovu walifanikiwa kuupata majira ya 8:00 usiku akiwa na majeraha ya kichwa.

Kwa upande wake daktari anayewahudumia majeruhi hao katika wodi ya mifupa hospital ya Mnazimmoja, Riffat Khalfan alisema, wamepokea majeruhi hao juzi Disemba 25 na kuwapatia huduma ya kwanza.

Alisema, kati ya wagonjwa wawili wapo katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na wawili wapo katika wodi za kawaida wakiendelea kupata matibabu.

Akiwataja wagonjwa waliokuwepo ICU alisema ni Haji Juma Machano (37) mkaazi wa Chumbuni na Dhamir Salum Dhamir (37) mkaazi wa Kinuni ambao hali zao bado hazipo vizuri na madaktari wanaendelea kuchukua jitihada ili kuhakikisha wananusuru maisha yao.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Lela Mohammed Mussa alisema serikali imeamua kuunda tume ya uchunguzi wa tukio hilo ili kuchunguza tukio la kuporomoka kwa jengo hilo.

Aliwaahidi wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuwa serikali itafanya jitihada ili kuhakikisha jengo hilo linarudi kama ilivyokuwa awali ili kuendelea kuwa nembo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.