LONDON, England
KOCHA wa Chelsea, Frank Lampard, amesema, kikosi chake hakiwezi kufanana na Liverpool ya msimu uliopita au Manchester City kwa ubora.

Lampard amesisitiza, Chelsea bado inajijenga na haoni kama msimu huu inaweza kuchukuwa ubingwa kwa kuangalia timu nyengine zinavyoonyesha viwango vikubwa.
Chelsea ilianza vizuri msimu ikawa kwenye nafasi tatu za juu, lakini, mambo yamevurugika kwenye michezo mitano ya mwisho ikishinda miwili, kufungwa miwili na kutoka sare mmoja na ikashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 22.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, mwanzoni mwa msimu aliwahi kusema Chelsea ina nafasi kubwa ya kuchukuwa ubingwa kutokana na mwenendo wake mzuri.
Lakini wiki kadhaa baada ya kauli hiyo, Chelsea walitolewa kwenye kinyang’anyiro kwa kupoteza michezo miwili ya Everton na Wolves.

“Siwezi kushinda kama Liverpool na ManCity ya misimu ya nyuma, kuna muda timu inapitia kwenye kipindi kigumu na unatakiwa uwe tayari kupokea hilo”.
“Kila mtu alikuwa anazungumzia kiwango chetu kizuri tulichoanza nacho. Kulikuwa na matumaini juu ya sisi kuchukuwa taji. “Wachezaji wangu wanatakiwa waendelee kujiamini”, alisema, Lampard.