NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imejikita katika kutafuta wafadhili kwa ajili ya kuwekeza kwenye vyanzo vipya vya utalii hasa katika mambo ya kale ambayo bado hayajatangazwa.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohammed Mussa aliyasema hayo wakati akizungumza na Zanzibar Leo huko ofisini kwake Kikwajuni Mjini Unguja.

Alisema serikali imeamua kutafuta wafadhili ili waweze kuwekeza na tayari wameshaonesha matumaini makubwa ya uwekezaji katika eneo hilo.

Aidha alisema tayari wizara imeshafanya mazungumzo na mmiliki wa hoteli ya Park Hayyat na Melia, Alisaid Albadawi ambae ni mwekezaji mkubwa barani Afrika, mashariki ya kati na nchi za Asia na mwengine kutoka nchi ya Amerika kutaka kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya kihistoria.

“Tumetafuta wafadhili ili waweze kuwekeza na tayari nimeshazungumza na wafadhili mbalimbali ambao wanaonesha matumaini ya kuwekeza katika eneo la Mkumbuni kisiwani Pemba ambao ni mji wa kale uliyopo chini ya bahari uliozama miaka mingi nyuma, Januari tumepanga tutaenda na tunatarajia mazungumzo yale yataleta baraka kwa kufungua fursa za kuwekeza,” alisema.

Waziri Lela alibainisha kwamba wawekezaji watasaidia sana kufanya matayarisho kuona wanasaidia kuwekeza katika maeneo hayo.

Hata hivyo, aliipongeza kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi juu ya dhamira yake ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa kisiwa cha uwekezaji na kutangaza kutoa punguzo maalum la uwekezaji hatua ambayo itafungua fursa kubwa kwa wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya Zanzibar.

“Tunajua ni muda mrefu litafanyika lakini hivi sasa tumeanza chini kuanza kutafuta wawekezaji kuanza mazungumzo ili kufikia azma yetu hii,” alisema.