PARIS, Ufaransa
MSHAMBULIAJI, Robert Lewandowski, baada ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa FIFA na kuwapiku Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, amedai, anahisi yupo katika kiwango kimoja wachezaji hao na sasa anaweza kuwaalika na kupata chakula pamoja.

Nyota huyo wa Bayern Munich ameyasema hayo katika mahojiano na ‘France Football’ ambapo pia aligusia namna yeye alivyonukia kutua United mwanzoni mwa kusakata kwake mchezo wa soka alipokuwa swali la mwandishi.

“Messi na Ronaldo hawa wamekaa katika meza moja, kileleni kabisa kwa muda mrefu na ndiyo sababu inawafanya watu kuwalinganisha.

“Kwa hiyo kwa kujibu suali lako, siwezi kuwa sawa nao kwa mtazamo huo. Baada ya tuzo, kama utachukua idadi kwa mwaka huu ama iliyopita hivi karibuni, nafikiri mimi nipo bora katika upande wa ‘kiwango’ na kwa idadi ya magoli.
“Nahisi kuwa meza moja na Messi na Ronaldo, nadhani naweza kuwaalika kupata chakula pamoja”.

Miaka miwili iliyopita, mchezaji wa Barcelona, Antoine Griezmann aliwahi kusema kwa kujilinganisha kuwa meza moja na Messi na Ronaldo katika uwezo. Lewandowski ametumia njia hiyo hiyo na yeye kujilinganisha na wachezaji hao wafalme wa soka kwa sasa duniani.

Wakati huo huo, Lewandowski alisema, ilikuwa bado kidogo tu kujiunga na Manchester United mwaka 2012 wakati wa kocha, Sir Alex Ferguson.
Mchezaji huyo wa Poland mwenye umri wa miaka 32 alisema, alifurahia mno msimu mzuri aliyokuwa akiitumikia Borussia Dortmund miaka 10 iliyopita.

Hata hivyo, alisema, United ilionyesha nia ya kumuhitaji na kuanza kushawishika zaidi ikiwa chini ya Ferguson ambaye alimfuata mwenyewe Lewandowsk kuzungumzia usajili wake.

Lewandowski amedai United ilikuwa imeanza mipango ya kukamilisha mpango huo.
”Baada ya mwaka wangu wa pili Dortmund, nilianza mazungumzo na Sir Alex Ferguson, alihitaji mimi niende Manchester”.