NA KHAMISUU ABDALLAH

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema serikali itahakikisha hospitali na vituo vya afya vya Zanzibar zinakuwa na dawa za kutosha.

Ameeleza kuwa hatua hiyo imelenga kuona wananchi wanaridhika na huduma zinazotolewa na dhamira ya serikali kustawisha afya za watu wake. 

Maalim Seif alitoa kauli hiyo wakati akiwajuilia hali wagonjwa waliolazwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja baada ya kupokea malalamiko ya kukosekana kwa dawa jambo linalopelekea kuzinunua katika maduka ya watu binafsi,

Alisema, sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwapatia matibabu wananchi wake bila ya malipo, hivyo aliwahakikishia kuwa atafuatilia suala hilo kwa lengo la kurekebisha kasoro zinazopelekea usumbufu kwa wagonjwa.

“Jambo hili huwezi kulaumu madaktari kwani wao lazima waletewe, tutahakikisha dawa na vifaa tiba vinakuja kwa wakati ili wananchi wetu wapate huduma nzuri na wazifurahie,” alisema.

Alibainisha kuwa hali hiyo inatokana na wizara kutotiliwa fedha kwa muda mrefu hivyo atahakikisha jambo hilo linatatuliwa mara moja ili kuondoa ugumu wa upatikanaji wa huduma. 

Aidha aliwaomba wagonjwa na jamaa zao kuwa na subira kwani serikali ya awamu ya nane haitaki kuona wananchi wanahangaika kutafuta matibabu.  

Aliwapongeza madaktari na wauguzi kuendelea kutoa matibabu mazuri kwa wagonjwa wanaofikishwa katika hospitali hiyo na kuwaomba kuzidisha jitihada kwani kazi ya udaktari ni kazi ya wito.

“Kazi hii inahitaji mtu awe na huruma katika kuwahudumia wagonjwa wetu, nami naamini nyinyi mmeonesha moyo huo kuona wagonjwa wetu mnawaangalia vizuri na mtauendeleza kwa maslahi ya taifa letu,” alisema.

Hata hivyo Makamu huyo aliwasisitiza madaktari wa hospitali zote nchini, kutekeleza wajibu wao kwa umahiri na misingi ya taaluma yao ili kuondoa malalamiko ya wananchi dhidi yao.

Akizungumza katika ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Mnazimmoja, Dk. Marijani Msafiri Marijani, alimuhakikishia Makamu wa rais kuwa wataendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa na wananchi ili wapate nafuu na kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa.