WASHINGTON,MAREKANI

MAUAJI mengine ya Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika yaliyofanywa na polisi nchini Marekani, yamechochea maandamano makubwa kupinga dhuluma za ubaguzi na ukatili wa polisi.

Andre Maurice Hill mwenye umri wa miaka 47 alipigwa risasi mara kadhaa na polisi, akiwa nyumbani kwake mjini Columbus, jimbo la Ohio, usiku wa kuamkia Jumatatu.

Polisi hao waliitwa kwenye eneo hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni tukio dogo.

Sekunde chache kabla ya kuanza kumiminiwa risasi, picha za video kutoka kamera ya polisi zinaonesha kuwa Hill alikuwa akiwafuata polisi akiwa na simu mkononi mwake.

Mkuu wa polisi wa Columbus, Thomas Quinlan, alitangaza kwamba atamfuta kazi Ofisa wa polisi aliyehusika na mauaji hayo, Adam Coy, kwa tuhuma za uvunjaji mkubwa wa maadili ya jeshi la polisi.

Mamia ya watu walijitokeza kwenye maandamano wakibeba mabango yaliyoandikwa, Maisha ya Mtu Mweusi yana thamani.

Hill ni Mmarekani mweusi wa pili asiye na silaha kuuawa na polisi kwa mwezi huu.