NA NIZAR VISRAM, OTTAWA

WAFANYAKAZI takriban milioni 250 nchini India waligoma mnamo Novemba 26 mwaka huu. Mgomo huu wa siku moja uliitishwa na vyama 10 vya wafanyakazi pamoja na jumuiya zaidi ya 250 za wakulima nchini humo. 

Wakati huohuo zaidi ya watu milioni 10 walishiriki maandamano yaliyofanyika nchini kote India. Kwa mujibu wa shirika la kazi duniani (ILO), mgomo kama huu haujawahi kufanyika katika historia ya India na hata kwengineko. 

Lengo lilikuwa ni kuwaunga mkono wakulima wa India wanaopinga sheria zilizopitishwa na serikali ya waziri mkuu Narendra Modi zitakazoruhusu sekta ya kilimo kudhibitiwa na kampuni kubwa.

Ilipofika Novemba 30 maelfu ya wakulima kutoka majimbo ya Punjab, Haryana, Uttarakhand na Uttar Pradesh waliandamana kuelekea mji mkuu wa Delhi. Polisi waliweka vizuizi barabarani ili kuwazuia wasiingie jijini Delhi.

Hata hivyo wakaamua kukaa barabarani wakila na kulala hapo hapo. Polisi walitumia mabomu ya machozi na marungu pamoja na maji ya kuwasha, lakini hawakufua dafu.

Waziri kiongozi wa Delhi, Arvind Kejriwal aliwatembelea wakulima waliopiga kambi nje ya jiji. Mara moja serikali kuu ikamuadhibu kwa kumfungia nyumbani kwake asitoke. Kejriwal ni kiongozi wa chama cha upinzani cha AAP kilichoshinda jijini Delhi.

Muigizaji wa sinema Deep Sidhu aliyekuwa miongoni mwa wakulima alimwambia ofisa wa polisi “Mheshimiwa, haya ni mapinduzi. Ukiwapokonya wakulima ardhi yao unafikiri wataishije?”.

Muigizaji na mwimbaji mwengine ni Diljit Dosanjh ambaye pia alishirikiana na wakulima. Inasemekana alitoa mchango wa rupia 100,000 kuwanunulia mablanketi ili kujikinga na ubaridi wa Delhi.

Muigizaji mashuhuri Priyanka Chopra naye ameunga mkono maandamano. Katika ukurasa wake wa Twitter ameandika: “Wakulima wetu ni askari wa chakula wa India. Hofu yao inahitaji kuondolewa. Matumaini yao yanahitaji kutimizwa. Tuhakikishe kuwa mgogoro huu umesuluhishwa mapema.”

Aliyekuwa waziri kiongozi wa jimbo la Punjab, Parkash Singh Badal aliamua kurejesha nishani ya heshima ya kitaifa kama ishara ya kuwaunga mkono wakulima “waliosalitiwa” na serikali. Aidha chama chake kilivunja ushirikiano na chama tawala cha BJP.

Badal aliungwa mkono na wanariadha takriban 150 walioshinda medali za Olympic. Wao waliamua kwenda ikulu ya Delhi ili kurejesha nishani za heshima walizotunukiwa na rais wa nchi

Wakulima wa India waliungwa mkono hata nje ya nchi. Katika mji mkuu wa London (Uingereza) mamia ya waandamanaji walikusanyika tarehe 6 Disemba nje ya ubalozi wa India. Barabara ilibidi ifungwe na polisi wakawakamata waandamanaji kadha.

Katika mji wa Winnipeg (Canada) watu waliandamana barabarani wakiwa katika magari yao. Kutokana na Corona na marufuku ya mkusanyiko ilibidi watumie magari ili kudhihirisha wanawaunga mkono wakulima wa India. Maandamano kama hayo yalifanyika pia katika miji ya Toronto, Saskatoon na Halifax nchini Canada.

Na waziri mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau alipoulizwa kuhusu wakulima wa India alisema Canada daima inaunga mkono haki ya wananchi kuandamana kwa amani popote duniani. Serikali ya India ikakasirishwa na kusema Trudeau anaingilia mambo ya ndani ya India.

Na nchini Australia nako, wananchi waliandamana nje ya ubalozo wa India mjini Melbourne.

Nchini India wakulima wamewasilisha kesi katika mahakama kuu wakiomba sheria tatu kuhusu wakulima zibatilishwe. Waliiambia mahakama kuwa sheria hizo zilipitishwa na serikali kwa kuburuzwa, bila kushauriana na wakulima ambao ni wadau wakuu. Wadau wengine ambao hawakushirikishwa ni serikali za majimbo ambazo kikatiba zina mamlaka ya kusimamia kilimo katika majimbo yao

Sheria hizo zilipitishwa kwa haraka katika bunge (Lok Sabha) mnamo Septemba kisha ikapelekwa katika baraza la juu (Rajya Sabha) ambako ilipitishwa kwa kutamka “ndiyo” tu bila ya kujadiliwa au kupigiwa kura.

Serikali imekataa kuzifuta sheria tatu na badala yake ilipendekeza kufanya marekebisho madogo. Sababu ilizotoa ni kuwa inabidi kukaribisha wawekezaji wakubwa katika sekta ya kilimo ili “kuleta maendeleo”.

Wakulima nao wamekataa marekibisho hayo na wameamua kuendelea na mgomo wao nje ya Delhi. Wamesema wataendelea kufunga barabara zinazoingia Delhi kwa sababu chini ya sheria mpya watalazimika kuuza mazao yao kwa makampuni binafsi kwa bei itakayopangwa na makampuni hayo.

Wanataka waendelee kuuza kwa bei itakayopangwa na kutangazwa na serikali. Kwa njia hii wamekuwa na uhakika wa bei na kwa hiyo wanahamasika kuzalisha wakijua hawatalanguliwa na matajiri.

Tarehe 9 Disemba serikali ilifanya mazungumzo na viongozi wa wakulima lakini hakuna muwafaka uliofikiwa. Hii ilikuwa ni mara ya tano mkutano kama huo kufanyika bila ya mafanikio

Sheria tatu zilizozpitishwa mnamo Septemba zinawafanya wakulima wasiwe na uhakika wa bei.  Ikumbukwe kuwa India inategemea sana kilimo. Kati ya jumla ya watu bilioni 1.4 takriban theluthi mbili wanategemea kilimo kwa maisha yao ya kila siku. Wengi wao ni wakilima wadogo weye mashamba yasiyozidi eka tano,

India ilipopata uhuru mwaka 1947 ilirithi kilimo cha kikoloni. Ilikuwa inaagiza chakula kutoka nje. Miaka ya 1965 hadi 1967 nchi ikakabiliwa na ukame na njaa kali. Ikabidi kuomba msaada wa chakula kutoka Marekani.

Baada ya miaka hiyo serikali ikaanzisha sera kabambe ili kujitosheleza kwa chakula. Maslahi ya wakulima na walaji ikaangaliwa na serikali ikatoa ruzuku kwa ajili ya mbolea, mbegu, jenereta, na mabomba ya umwagiliaji.

Serikali ikapanga bei muwafaka kwa mkulima aliyehakikishiwa soko la mazao yake (mandi kwa Kihindi). Katika muda usiozidi miaka kumi uzazilashi ukaongezeka maradufu 

Si India tu bali hata nchi za Kiafrika zililazimishwa zilime mazao ya biashara kwa ajili ya masoko ya Ulaya badala ya mahitaji yetu. Tukawa tunalima pamba, mkonge na kahawa na kuuza Ulaya halafu tunaagiza mchele, ngano na sukari kutoka nje.

Wengine tunakumbuka jinsi Mwalimu Nyerere alivyoshinikizwa na wakopeshaji na “wafadhili” kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) tuache kutoa ruzuku kwa wakulima na tuvunje vyama vya ushririka. Bunge letu likaambiwa kila mtu atabeba msalaba wake.

Pale tunapotaka kufanya mageuzi ya kimfumo nchi za kibeberu zinakuja juu. Wanaanza kutushitaki katika shirika la biashara duniani (World Trade Organization – WTO). Kikao chao kinaitwa Doha Round.

Katika kikao hiki India ikatiwa msukosuko na Marekani. Wakasema sera mpya ya India ya kujitosheleza kwa chakula eti inakwenda kinyume na sera yao ya soko huriya na kwa hiyo wanapaswa kuachia soko liamue bei ya nafaka.

Profesa Prabhat Patnaik wa India anasema enzi hizo za Nehru na Indira Gandhi India ilikuwa na jeuri ya kuweza kukabiliana na ubeberu katika Doha Round, lakini leo jeuri hiyo imepotea. Anasema serikali ya leo “ama inaogopa au haielewi jinsi ya kukabiliana na ubeberu.”

Patnaik anaongeza, ndipo leo tunasikia lugha kama “maendeleo ya kilimo” au “kilimo cha kisasa” ikitumiwa wakati malengo yake ni tofauti. Kinachofanyika ni kuwa India inarudia kilimo cha kikoloni ambapo mazao ya chakula yanaporomoka na ardhi inadhibitiwa na makampuni makubwa, anasema profesa huyo mchumi.

Ukweli ni kuwa pato la mkulima wa India lilikuwa linaanguka hata kabla waziri mkuu Modi kuingia madarakani mwaka 2014. Ndio maana wakulima walimuunga mkono alipowaahidi kuwa katika muda wa miaka mitano ya utawala wake pato lao lingeongezeka maradufu. Alisema serikali yake itapanga bei ya mazao yao asilimia 50 zaidi ya gharama za uzalishaji 

Miaka mitano ilipita na wakulima hawakuona ahadi ikitekelezwa. Badala yake bei wanayopewa ni pungufu kuliko gharama ya uzalishaji. Mazao ya kilimo yalikuwa yanachangia asilimia 33 katika uchumi wa taifa (GDP), leo ni asilimia 15

Nusu ya wakulima wameelemewa na madeni. Miaka ya 2018 na 2019 wakulima zaidi ya 20,600 walilazimika kujinyonga, kwa mujibu wa shirika la jinai (National Crime Records Bureau)

Ndipo imefikia mgomo huu wa muda mrefu ambao huenda ukaathiri uchumi wa nchi na kusababisha ukosefu wa chakula.

Wakati naandika haya mgomo wa wakulima unakaribia mwezi mmoja na hakuna ishara ya kumalizika. Mahakama kuu imesema wakulima hao wana haki ya kugoma mradi tu hawamshambulii mtu wala kuharibu mali ya mtu

nizar1941@gmail.com