Wataka jamii isijisahau kujikinga na corona

 NA KIJA  ELIAS, MOSHI

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mhashamu Ludovick Joseph Minde, amewataka Watanzania kuitumia Sikukuu ya Krismasi ya mwaka huu, kuwaombea wenzao sehemu mbalimbali duniani ambao hawakuweza kuisherehekea kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili. 

Mhashamu Ludovick Minde, alitoa wito huo jana, wakati akitoa salamu zake za Krismasi katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika Kanisa la Kristo Mfalme, mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Askofu Minde, alisema hali sio nzuri katika ya baadhi maeneo hapa duniani kutoka na kuendelea kuweko changamoto mbalimbali ikiwepo ile ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona. 

“Kuna wenzetu huko Ulaya, India, Marekani na sehemu nyengine ambao hawakupata fursa ya kusherehekea Noeli ya mwaka huu, wako katika hali mbaya, hawawezi kujumuika kwa pamoja kama tulivyofanya sisi mkesha wa kuamkia leo na Asubuhi hii, tuwaombee ili Mwenyezi Mungu awajalie kheri kuepuka majanga yanayowakabili”, alisema. 

Aidha alitoa rai kwa Waamini wa Jimbo Katoliki Moshi, kumuombea Hayati Askofu Anthony Banzi, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga, aliyefariki hivi karibuni na ambaye alisema anatarajiwa kuzikwa wiki ijayo, ambapo pia aliwataka kuwaombea Waamini wenzao wa Jimbo Katoliki Tanga kuwa na subira katika kipindi hiki wanachoomboleza kifo cha kiongozi wao wa kiroho.

Kuhusu Sikukuu ya Krismas, Askofu Ludovick Minde, ambaye pia ni Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki Kahama, alisema siku hiyo ni kumbukumbu ya kipekee inayowakumbusha wanadamu umuhimu wa kuwa na amani, upendo na mshikamano miongoni mwao, ambapo alitoa rai kwa waamini wote kuifanya Sikukuu hiyo kuwa ya kifamilia zaidi kwa waamini kuungana na wanafamilia wenzao kuisherehekea kwa amani.