LONDON, England
LIGI Kuu ya England ambayo imeshamiri kutokana na urahisi wa sheria za uhamiaji ndani ya Umoja wa Ulaya, inatarajia kuanza kuona mabadiliko kuanzia mwakani, baada ya Brexit kuanza kutekelezwa.


Utaratibu wa sasa ambao unaruhusu makocha wa Ujerumani kushirikiana na makocha wa mazoezi kutoka Ureno, kufundisha soka kama ya Hispania kwenye viwanja vya England, umekuwa msingi wa ukuaji wa soka nchini humo.


Hali hiyo itaanza kubadilika baada ya Brexit kuanza kutekelezwa. Kuanzia Januari raia wa nchi nyengine za Ulaya watahitaji kufanya ‘visa’ ili kucheza England.


Bado haijulikani ni vigezo gani hasa vitafuatwa, lakini, kwa ujumla utakuwa ni utaratibu kama unaofuatwa kwa nchi nyengine zote duniani.


Sheria mpya zitakuwa na athari mbili za haraka, ya kwanza, kwamba wachezaji kutoka nchi za Umoja wa Ulaya wanaotarajia kucheza England watashughulikiwa kwa njia sawa na wachezaji kutoka ulimwengu kote.


Lakini, wachezaji hawatakuwa na shida kuingia kama ‘CV’ zitathibitika kuwa zinavutia vya kutosha.(AFP).