NA ASYA HASSAN

MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, amewasisitiza Madiwani wa Wilaya ya Kusini Unguja, kutojishirikisha katika masuala ya migogoro ya ardhi , rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, kwani kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi wa nchi na kuzofisha upatikanaji wa maendeleo.

Mkuu huyo, alisema hayo alipokuwa akifunguwa kikao cha Madiwani kilichoambatana na uchaguzi wa kuchagua Mwenyekiti, atakaeweza kuongoza Baraza la Madiwani hao kwa kipindi cha miaka mitano, kikao ambacho kilifanyika katika Ofisi ya Halmashauri Kitogani wilaya ya Kusini Unguja.

Alisema wananchi wamewapa dhamana za kuwatumikia hivyo wasitumie nyadhifa hizo kwa kujinufaisha wao binafsi na kusahau dhamana walizopewa.

Hata hivyo, Mkuu huyo, alifahamisha kwamba serikali ya awamu ya nane imekuwa ikisisitiza viongozi kuwa wabunifu na kuwatumikia wananchi ipasavyo, ili kupatikana maendeleo.

Kwa upande wa uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Madiwani wamemchagua Mustafa Ali Hamadi kuwa Mwenyekiti mpya wa baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa Mwenyekiti huyo, alisema katika kipindi hichi cha uongozi wake baraza litahakikisha linasimamia kikamilifu masuala mbali mbali ya huduma za kijamii.

Akitaja baadhi ya huduma hizo, alisema ni pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuimarisha huduma muhimu za kijamii ikiwemo afya, elimu na usafi, ili kuona azma ya serikali ya awamu ya nane ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi inafikiwa.

Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kuwataka madiwani kuwa karibu na wananchi katika kuwasaidia kubuni njia za miradi ya maendeleo itakayoleta tija kwao na taifa.

Pamoja na mambo mengine baraza hilo lilijadili na kupitisha

mambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya fedha za mradi wa uvuvi , ambapo mratibu wa mradi huo kutoka halmashauri ya wilaya hiyo Ali Abdallah, alisema zaidi ya shilingi milioni 100 zimetolewa kupitia ufadhili wa shirika la UNCDF ikiwa ni mtaji utakao ekeza katika mradi huo kwa miaka mitano ambao unalenga makundi ya kinamama na vijana.