NA KHAMISUU ABDALLAH

BEI za bidhaa ya mafuta kwa mwezi huu imepungua kutokana na kubadilika kwa wastani wa bei za bidhaa hizo katika soko la dunia.

Akizungumza na Zanzibar leo ofisini kwake Maisara, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kutoka Mamlaka ya Udhitibi wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Mbarak Hassan Haji alisema mafuta ya petroli kwa mwezi huu yamepungua kutoka shilingi 1,948 hadi shilingi 1,912 sawa na asilimia 1.85.

Aidha alisema mafuta ya dizeli yameshuka kutoka shilingi 1,866 kwa mwezi uliopita hadi shilingi 1,820 kwa mwezi huu ambayo yamepungua kwa 46 sawa na asilimia 2.47.

Kwa upande wa mafuta ya taa Mbarak, alisema bei ya reja reja ya mafuta ya taa kwa mwezi huu ni shilingi 1,233 sawa na asilimia 23.23 ukilinganisha na mwezi uliopita ambayo yalikuwa yakiuzwa kwa shilingi 1,606.

Hata hivyo, akizungumzia sababu nyengine zilizopelekea kushuka kwa bei za mafuta kwa mwezi huu alisema ni soko la ndani kwa kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Hivyo, aliwaomba wananchi kuwa bei zilizotangazwa na serikali ndio bei halali huku akitumia muda huo kuwasisitiza kununua mafuta katika vituo halali vya mafuta na kudai risiti pale wanapouziwa nishati hiyo.

Sambamba na hayo aliwasisitiza wafanyabiashara wa bidhaa hiyo katika sheli kuhakikisha wanatumia bei zinazotangazwa na mamlaka hiyo kwani zipo kisheria.