PRISHTINA, KOSOVO

MAHAKAMA ya kikatiba ya Kosovo imetoa uamuzi ambao utalazimisha kufanyika uchaguzi mpya nchini humo.

Jaji aligundua kuwa uchaguzi uliompa ushindi waziri mkuu wa sasa,Avdullah Hoti, ulikiuka sheria. Hoti alichaguliwa kwa idadi ndogo ya kura 61 kati ya wabunge 120.

Uamuzi huo mpya wa mahakama unasema kuwa uchaguzi wa Hoti haukuwa halali, kwa sababu mmoja wa wabunge waliompigia kura hakustahiki kufanya hivyo.

Mwanasiasa huyo alikutwa na hatia ya kosa la udanganyifu wakati wa kupiga kura.

Mwishoni mwa mwezi Septemba, alianza kutumikia kifungo chake gerezani.

Rais wa sasa, Vjosa Osmani, atakutana na wawakilishi wa chama kuamua tarehe mpya ya uchaguzi, kulingana na ripoti za vyombo vya habari. Uchaguzi mpya lazima ufanyike ndani ya siku 40.