NEW YORK, MAREKANI

MAHAKAMA ya rufaa nchini Marekani imekubaliana na uamuzi wa kufuta kesi iliyofunguliwa na upande wa Rais Donald Trump uliotaka kiongozi huyo atangazwe mshindi wa jimbo Wisconsin.
Mpinzani wake, Joe Biden kutoka chama cha Democrat, alishinda kwa ushindi mdogo wa asilimia 0.6 katika uchaguzi wa mwanzoni mwa mwezi uliopita,lakini ulikuwa muhimu kuchangia kwenye safari yake ya kuingia Ikulu ya White House.
Mwanzoni mwa mwezi huu,Trump alifunguwa kesi dhidi ya tume ya uchaguzi,akiitaka mahakama iliamuru bunge la jimbo hilo ambalo linatawaliwa na chama chake limtangaze yeye mshindi, lakini Jaji Brett Ludwig alikataa hoja hiyo.
Uamuzi wa mahakama ya rufaa iliyoongozwa na majaji watatu, wote wakiwa wameteuliwa na marais kutoka chama cha Republican, chake Rais Trump, unaongeza idadi ya kesi za uchaguzi, ambazo Trump ameshindwa.