NA MARYAM HASSAN

MMOJA kati ya majeruhi wanne wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la Beit al Ajaib amepelekwa katika hospitali ya Muhimbili jijini dar es salam kwa matibabu zaidi.

Akizungumza na Zanzibar leo Msemaji wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Hassan Makame Mcha, amesema uongozi wa hospitali hiyo umeridhia kusafirishwa kwa mgonjwa huyo.

Alimtaja majeruhi huyo kuwa ni Haji Juma Machano (37), mkaazi wa Chumbuni, wilaya ya mjini unguja ambae amesafirishwa juzi kutokana na majeraha aliyoyapata katika ajali hiyo.

 “Si kama hapa tumeshindwa lakini kwa hali aliyokuwa nayo imelazimika tumsafirishe kwa ajili ya matibabu Zaidi,” alisema Mcha.

Aliongeza kuwa katika ajali hiyo majeruhi huyo aliathirika zaidi sehemu ya ini na kupelekea kufanyiwa upasuaji kabla ya kusafirishwa ili kupatiwa matibabu zaidi ya kibingwa katika hospitali ya rufaa ya muhimbili.

Aidha mcha alieleza kuwa majeruhi mwengine wa ajali hiyo Ali Ramadhani Juma, ameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya hali yake kuimarika licha ya madaktari kuendelea kufuatilia afya yake akiwa nyumbani.

“Licha ya kupewa ruhusa, tutahakikisha kuwa tunafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya afya yake ili kama atakutwa na tatizo lolote madaktari watampatia huduma kwa haraka zaidi”, alieleza Mcha.

Akizungumzia hali ya majeruhi mwengine Dhamir Salum Dhamir (37), mkaazi wa Kinuni, alisema anaendelea vyema licha ya kuendelea kuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

“Bado yupo ICU lakini Sasa hali yake inaendelea kuimarika kwani madaktari wapo karibu sana na mgonjwa huyu kwa ajili ya matibabu yake,” aliongeza.

Jengo la kihistoria la Beit al Ajaib liliporomoka Disemba 25 mwaka huu na kupelekea vifo vya watu wawili na majeruhi wanne ambao walikuwa mafundi na vibarua waliokuwa wakiendelea na ukarabati wa jengo hilo.