NA MARYAM HASSAN

KIJANA Nassor Ame Haji (27) mkaazi wa Jumbi, amehukumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka 19, mara baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matano ikiwemo wizi.

Kijana hiyo amepokea adhabu hiyo katika mahakama ya mkoa Mwera, chini ya Hakimu Said Hemd Khalfan, kwa kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Hakimu huyo alisema, kwa kosa la kuvunja nyumba ya kuishi usiku kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi ndani humo, atumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka saba.

Kosa hilo anadaiwa kutenda Disemba 12 mwaka 2018 baina ya saa 8:00 za usiku hadi saa 11:00 za alfajiri, huko Tunguu Suza wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa huyo alivunja nyumba ya kuishi Ahmed Abdi Bakari, kwa nia ya kutenda kosa la wizi ndani humo jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aidha alisema, kosa la wizi alilodaiwa kutenda siku hiyo kwa kuiba simu moja aina ya Tacno Y3+ rangi ya blue kwa weusi yenye thamani ya shilingi 90,000 mali ya Swalha Khamis Hamad, amemtaka kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka mitatu.

Aidha Nassor anadaiwa kutenda tena kosa la wizi katika nyumba hiyo kwa kuiba mkoba mmoja wa rasket rangi nyeusi, kipochi kimoja rangi nyeusi kwa dhahabu, flash moja nyeusi, pete tatu, kufuli moja yenye funguo mbili, sarafu moja ya zamani ikiwa na maandishi ya kiarabu.

Vyote hivyo vikiwa na thamani ya shilingi 2,42,000 kwa kukisia mali ya Khaitham Rajab Khatib, jambo ambalo ni kosa kisheria, katika kosa hilo pia mshitakiwa ametakiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka mitatu.

Aidha kosa la nne pia mshitakiwa ametakiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka mitatu, ambalo ni kosa la wizi alilodaiwa kutenda siku hiyo hiyo.

Ilidaiwa kuwa, mshitakiwa aliiba laptop moja aina ya Toshiba yenye thamani ya shilingi 450,000 kwa makisio mali ya Khadija Talib Riziwani, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Pamoja na hayo mshitakiwa katika kosa la tano nalo pia ametakiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka miatatu.

Kwa adhabu hiyo, mshitakiwa anadaiwa kuiba simu moja aina ya Tecno F1 yenye rangi cream kwa weusi yenye thamani ya shilingi 150,000 kwa makisio mali ya Rehema Juma Mzee, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ayoub Nassor Sharif, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa kuwa hana kumbu kumbu ya makosa ya zamani dhidi ya mshitakiwa huyo.

Kwa upande wa mshitakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ni tegemezi katika familia na pia ni kosa lake la kwanza.

Aidha amesema ikiwa haitowezekana mahakama impe adhabu mbadala.

Katika kesi hiyo ilifunguliwa Januari 9 na kuanza kusikilizwa ushahidi Januari 23 mwaka jana na jumla ya mashahidi watano walisikilizwa ushahidi.