NA LAILA BAKAR

IDARA ya Makumbusho na Mambo ya Kale Zanzibar imeilalamikia Idara ya ardhi kutokuwapa mashirikiano ya kutosha juu ya kutatuta migogoro ya ardhi inayoendelea kujitokeza katika maeneo ya kihistoria.

 Akizungumza na gazeti hili Ofisa wa Makumbusho na mambo ya kale Zanzibar, Ali Ussi Ali, alisema hali hiyo imejitokeza baada ya kukubaliana na maafisa wa ardhi kwenda kutatua mgogoro wa ardhi, uliopo katika eneo la kisima cha chini kwa chini, kilichopo Mangapwani Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja matokeo yake Maafisa hao hawakufika katika eneo hilo.

Alisema mgogoro huo umetokea baada ya mwananchi mmoja kudai eneo la kisima hicho liliopo katika sehemu ya shamba lake analomiliki na vielelezo vyote anavyo.

Hivyo Ofisa huyo alitumia fursa hiyo kuiomba Idara ya ardhi kutoa mashirikiano ya kina, ili kuweza kufanikisha kutatua mgogoro huo kwa usalama.

Nae Mhandisi Majenzi wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya kale Zanzibar, Saada Mussa Said, alisema si vyema kwa watumishi wa umma kupuuza ahadi, kwani kufanya hivyo kunasababisha kuzorotesha baadhi ya kazi kushindwa kutekelezwa kwa wakati.

Alifahamisha kwamba maeneo ya kihistoria yamekuwa na malalamiko mengi ya kuvamiwa na wananchi, hivyo alitumia fursa hiyo kuisisitiza Idara ya Ardhi kutoa ushirikiano wa kina juu ya kutatua migogoro ya ardhi inayoendelea kujitokeza katika maeneo ya makumbusho ambayo ni urithi wa dunia.