NA ASYA HASSAN

UONGOZI wa Jimbo la Malindi umesema utaandaa kambi maalum za huduma za afya kupitia shehia mbalimbali zilizopo ndani ya jimbo hilo kwa kila baada ya miezi mitatu.

Akizungumza katika kambi ya siku moja ya kupima huduma za afya huko mapembeani Mwakilishi wa Jimbo hilo, Mohammed Ahmada Salum, alisema hatua hiyo itasaidia jamii kujua afya zao.

Alisema ndani ya jimbo hilo kuna wazee wenye umri mkubwa ambao wanaugua maradhi mbalimbali na hawana uwezo wa kwenda vituo vya afya kuangalia afya zao hivyo kupitia kambi hizo itakuwa chachu ya kuwasaidia na kujua afya zao kwa wakati.

Mwakilishi huyo alifahamisha kwamba kupitia kambi hizo watahakikisha wanakuwepo wataalamu wa maradhi tofauti ili kuwasaidia wananchi hao kujua tatizo linalowasumbua na kupata huduma za afya bila ya usumbufu.

Alifahamisha kwamba ili wananchi waweze kufanya shughuli zao za kimaendeleo na kulijenga taifa wanahitaji kuwa na afya imara, jambo litakalosukuma juhudi za kuinua uchumi wa nchi.

Hivyo Mwakilishi huyo, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi hao zitapowekwa kambi hizo kuzitumua ipasavyo, ili ziweze kutoa tija kwao na taifa kwa ujumla.

Nae mwenyekiti wa jumuiya ya Mwembetanga Youth Organization, Mohammed Juma Salum, aliwaomba vijana kunapokuwa na kambi kama hizo kuwa na utamaduni wa kwenda kujitolea, kwani kambi hizo zinawasaidia kupata ujuzi na kuisaidia jamii.

Alifahamisha kwamba asilimia kubwa ya vijana hawako tayari kujitolea katika harakati za kimaendeleo, jambo ambalo linasababisha kudidimiza maendeleo ya nchi.

Kwa upande wa wananchi hao waliomba huduma hizo ziwe endelevu kwani zinawasaidia wananchi kujua afya zao na kuondokana na wasiwasi.

Kambi hiyo ya siku moja inayotoa huduma za presha, sukari, uzito, ushauri nasaha imeandaliwa na uongozi wa jimbo hilo ambapo zadi ya watu 100 wamejitokeza kuangalia afya zao.