BEIJING,CHINA

WIZARA ya Ulinzi ya Taiwan imesema kundi la manowari za China za kubeba ndege limepita kwenye mlango bahari ya Taiwan.

Upitaji huo unakuja siku moja baada ya meli ya kivita ya Marekani kupita kwenye njia hiyo ya majini.

Wizara hiyo ilisema kuwa meli hizo zilianza safari kutoka kwenye mji wa kaskazini mashariki mwa China wa Dalian siku ya Alhamisi na kupita kwenye mlango bahari huo kutoka kaskazini kuelekea kusini.

Taiwan ilisema jeshi lake limetuma meli na ndege ili kulinda na kufuatilia safari za meli za China.

Safari hizo za manowari zinakuja wakati ambapo China ilikuwa ikiongeza shughuli za jeshi lake katika maeneo yaliyo jirani na Taiwan ukiwemo mlango bahari ya Taiwan.

Wakati huo huo, Jeshi la Majini la Marekani linasema manowari yake ya kundi la saba iitwayo USS Mustin ilifanya safari za kawaida ikipita kwenye mlango wa bahari ya Taiwan.

Vyombo vya habari vya Taiwan vilisema hiyo ilikuwa ni misheni ya 12 kufanywa na Jeshi la Majini la Marekani mwaka huu.