NA KHAMISUU ABDALLAH
TAMASHA la saba la maonesho ya biashara linatarajia kufanyika kuanzia Januari 4 mwakani katika viwanja vya Maisara ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Masoko wa wizara hiyo, Khamis Ahmada Shauri, ameliambia gazeti hili kwamba tamasha hilo litafanyika kwa siku 10 na litafungwa rasmi Januari 15 mwaka huu.

Alisema tamasha hilo la kila mwaka limelenga kutoa fursa mbali mbali ikiwemo kuzitangaza huduma, biashara na bidhaa zinazozalishwa nchini kutambulika katika masoko ya kitaifa na kimataifa.

Alisema katika tamasha hilo zaidi ya washiriki 360 kutoka ndani na nje ya Zanzibar wanatarajiwa kushiriki tamasha hilo na kwamba idadi hiyo imeongezeka kutokana na kuongezeka kwa washiriki kutoka nje ya Zanzibar.

“Wizara imeshaanza matayarisho ya tamasha hilo na miundombinu katika eneo la maonesho itaanza kuwekwa rasmi Disemba 28 mwaka huu ikiwemo kufunga mabanda,” alieleza Shauri.

Alisema wizara kwa kawaida imekuwa ikipokea washiriki kutoka nje ya Zanzibar ikiwemo Kenya, Burundi, Rwanda, Uganda, Siria, Uturuki na nchi nyengine lakini kutokana na uwepo wa maradhi ya corona zipo nchi hazitoshiriki.

Alisema hali hiyo inatokana na baadhi ya nchi hazijafungua mipaka ya nchi zao ingawa wamepata washiriki kutoa nchi za Burundi na Kenya huku wageni wa nje wanaofanya biashara zao Tanzania bara wameshaonesha mwitikio mzuri.

Akizungumzia mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha hilo alisema mpaka sasa wizara inaendelea na mchakato huo lakini wanategemea mmoja kati ya viongozi wakubwa nchini atafungua maonesho hayo.

Hivyo, aliwaomba wafanyabiashara kushiriki katika kuonesha biashara zao na kuwataka kuchukua risiti zao zilizoonesha kulipia kodi ya serikali.

“Mara hii itakuwa tofauti na matamasha mengine yaliyopita kwani serikali itataka kukusanya mapato yake kupitia kodi mbalimbali ni vyema kwa wafanyabiashara kuzingatia jambo hili,” alisisitiza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Juma Hassan Reli, alisema dhamira ya serikali kuweka tamasha hilo kila mwaka katika kuelekea sherehe za Mapinduzi ni kutangaza bidhaa na kubadilishana uzoefu na teknolojia baina ya wafanyabiashara wa Zanzibar na wanaotoka nje.

Alisema hatua hiyo pia imesaidia kukua kwa sekta hiyo na kutoa fursa kadhaa kwa wananchi ambazo zinapelekea kuchochea ukuwaji wa pato la taifa.

Mbali na hayo, alibainisha kuwa maonesho hayo pia yatashirikisha taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya huduma wanazozitoa na kwamba wizara imeshatangaza maonesho hayo katika mitandao na kutegemea taasisi za Tanzania bara zitashiriki katika tamasha hilo.

Hivyo, alizishauri taasisi za serikali ambazo bado hawajapeleka maombi ya kushiriki kwao kujiandikisha mapema ili waweze kupatiwa mabanda kutokana na muitikio mkubwa wa washiriki na kuna uwezekano wa kukosa nafasi ya kushiriki.