TIGRAY, ETHIOPIA

MAPIGANO yameripotiwa kuendelea katika mkoa wa Tigray, karibu miezi miwili baada ya kuzuka vita katika jimbo hilo linalotaka kujitenga kutoka Ethiopia.

Serikali ya Ethiopia kwa wakati huu inachukua jitihada za kurejesha amani katika mkoa huo, lakini wapiganaji wa Tigray waliopambana na serikali bado wanaendeleza mapigano katika baadhi ya maeneo.

Hata hivyo misafara ya gari ya mashirika ya misaada ya kibinadamu imeendelea kuingiza misaada ya chakula, lakini hali bado ni tete na mawasiliano hasa ikizingatiwa kuwa hadi sasa mawasiliano yamekatwa.

Vikosi vya upinzani vya TPLF vinaendelea na vita, kutoka maeneo ya vijijini, wakati jeshi la Ethiopia linadhibiti miji kuu ya jimbo la Tigray, huku hofu  ikiendelea katika vijijini vya jimbo hilo.

Katika eneo la bara, bado ni ngumu kubaini ni maeneo yapi chini ya udhibiti wa serikali na ambayo yako mikononi mwa TPLF, chama kilichopinga Tigray kuwa mikononi mwa mamlaka ya serikali ya Addis Ababa.

Vyanzo kutoka mashirika ya kutoa misaada vinaripoti kuwepo na mapigano katika maeneo ya vijijini, hasa karibu na mji wa Shire, huku Umoja wa Mataifa ukisema mapigano yanaripotiwa mashariki mwa mji wa Mekele, mji mkuu wa jimbo la Tigray.

Taarifa hiyo imethibitishwa na wakaazi wa baadhi ya maeneo ya mji huo, ambao pia wamekiri kwamba eneo la kaskazini mwa jiji bado liko kwenye vita.

Ofisa mmoja wa serikali ya Ethiopia amekiri kwamba wanamgambo wa Tigray bado wanakabiliana na vikosi vya serikali. Serikali ya shirikisho imeanzisha utawala wa muda huko Tigray, ambayo inadai kuwa huduma za msingi zimeanza tena kutolewa.