Na HAFSA GOLO

SERIKLI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema itaadhimisha kutimia miaka 57 ya mapinduzi kwa aina ya kipekee iliyolenga kuongeza hamasa na kujenga uzalendo kwa wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili Rais, Sera Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohammed alieleza hayo jana alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Alisema maadhimisho hayo ya sherehe za mapinduzi kwa mwaka 2021, yatajenga hisia kwa wananchi juu ya mapinduzi hayo sambamba na kuendelea kujali uzalendo wao.

Dk. Khalid alisema katika maadhimisho hayo jumla ya miradi 12 itahusishwa ambapo kati ya hiyo mitatu itawekwa mawe ya msingi na tisa itafunguliwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Alisema zoezi hilo litahusisha viongozi wakuu wa kitaifa na mawaziri ndio watakuwa wageni rasmi katika shughuli hizo.

Aidha alisema kutakuwa na maonyesho ya biashara ya kitaifa yatakayofanyika katika viwanja vya Maisara ambapo sekta za umma na binafsi zitashiriki kikamilifu kuonyesha bidhaa na huduma wanazozitoa.

Kuhusu siku ya kilele cha mapinduzi ambayo ni Januari 12, alisema kutafanyika maonyesho ya amsha amsha ya mapinduzi yatakayofanywa na vikosi vyote vya ulinzi vilivyopo Zanzibar pamoja na wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar.

Alifahamisha kwamba maonyesho hayo yataanza katika viwanja vya Garagara Mtoni saa 12 asubuhi na kumalizika katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kwamba vikosi hivyo vitajigawa makundi matatu yatakayopita njia tatu tofauti.

Alizitaja njia hizo ni pamoja na njia ya Garagara- Maruhubi – Saateni – Ziwani Polisi ambapo njia ya pili itakuwa Garagara – Maruhubi – Darajani na Ziwani Polisi na njia ya Tatu itaanza pia Garagara –Darajabovu – Magomeni na Ziwani Polisi.

Waziri huyo. alisema mara baada ya kukamilika kwa maonyesho hayo vikosi hivyo vitaondoka Ziwani Polisi na kuwasili katika viwanja vya MnaziMmoja kwa mapokezi rasmi.

Hivyo aliwataka wananchi wote kukaa pembeni ya barabara vitakavyopita vikosi hivyo pamoja na kushiriki katika mapokezi hayo ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi atayapokea na kusoma salamu fupi.

Pamoja na maonyesho hayo pia kutakuwa na maandamano ya wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar ambayo yatapokelewa na Dk. Hussein saa 3 asubuhi.

Aidha alisema siku hiyo ya kilele Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi atahutubia taifa kwa kupitia vyombo vya habari.