NA MWAJUMA JUMA
TIMU ya soka ya wanawake ya Feature Queens imetoka kidedea mbele ya Ladies Queens kwa kuifunga bao 1-0 katika michuano ya kombe la Mapinduzi uliochezwa jana uwanja wa Mao Zedong.


Miamba hiyo ambayo ilishuka majira ya saa 10: 00 za jioni ulikuwa na ushindani na kutoa hamasa kwa watazamaji waliohudhuria uwanjani hapo.


Licha ya timu hizo kuwa wanagenzi lakini walionekana kucheza mchezo mzuri na kuonesha viwango vyao ambavyo wengi waliokuwepo hapo waliridhika navyo.


Bao hilo la pekee la Feature Queens liliwekwa kimiyani na mchezaji wao Nasra Abdalla Nyonje katika dakika ya 19 ikiwa ni dakika tatu tu baada ya mchezaji wao Siti Hemed kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mwanahija Makame .


Wakicheza kwa kila mmoja kumsoma mwenziwe miamba hiyo ilikwenda mapumziko kwa timu ya Feature Queens kuongoza kwa bao moja.


Timu hizo zilikianza kipindi cha pili kwa tahadhari sana na kuendelea kushambuliana lakini mashambulizi yao hayo hayakuweza kubadilisha matokeo hayo.


Ligi hiyo leo itaendelea tena kwa kuchezwa mchezo mmoja ambao utawakutanisha Amani Queens na Yellow Queens katika uwanja wa Mao Zedong saa 10: 00 za jioni.