WASHINGTON,MAREKANI

WIZARA ya Sheria ya Marekani imetangaza mashitaka dhidi ya ofisa mmoja wa zamani wa ujasusi wa Libya ambaye anadaiwa kutengeneza bomu lililoripuka ndani ya ndege ya Pan Am nambari 103 juu ya anga la Lockerbie, Scotland miaka 32 iliyopita.

Jumatatu Desemba 21, 2020 yalikuwa ni maadhimisho ya miaka 32 ya mripuko huo wa mwaka 1988, ambao uliangusha ndege hiyo kwenye anga ya Lockerbie na kuuwa watu wapatao 270.

Mwanasheria mkuu wa Marekani William Barr aliwaambia waandishi wa habari, kwamba ataletwa Marekani kwa ajili ya kesi hiyo .

Mwanasheria Mkuu wa Marekani William Barr alisema serikali ya nchi hiyo ina matumaini kwamba raia huyo wa Libya ambaye alishitakiwa katika shambulizi la bomu la ndege ya Pan Am nambari 103 mnamo mwaka 1988 atakabidhiwa kwa mamlaka nchini Libya.

Barr alitangaza mashitaka yanayohusiana na ugaidi dhidi ya Abu Agila Muhammad Mas’ud Kheir Al-Marimi kwa shutuma ya kushiriki kwake katika shambulizi lililouwa watu 259 ndani ya ndege na watu wengine 11 ardhini.

“Tunadhani matarajio ni mazuri sana. Masud yuko chini ya ulinzi wa serikali ya sasa ya Libya na hatuna sababu ya kufikiria serikali hiyo inavutiwa kujihusisha na kitendo hiki kibaya cha ugaidi, na hivyo tuna matumaini kwamba watamkabidhi ili kukabiliana na mkondo wa sheria.”alisema Barr.