LONDON,UINGEREZA
MAREKANI na Uingereza zimeelezea wasiwasi juu ya kesi ya wanaharakati wa Hong Kong wanaotuhumiwa kukimbilia Taiwan.
Wanaharakati 12 wanaopigania demokrasia walikamatwa na walinzi wa pwani wa China mwezi Agosti wakijaribu kuingia Taiwan kwa boti.
Baadaye walishitakiwa kwa kusafiri majini kinyume cha sheria,wengi wao walikuwa nje kwa dhamana baada ya kukamatwa au kushitakiwa kwa kuhusika katika maandamano ya kuipinga serikali huko Hong Kong.
Kesi ya wanaharakati kumi ilianza kusikilizwa Jumatatu katika mahakama moja iliyo katika mji wa kusini wa Shenzhen jirani na Hong Kong.
Wanadiplomasia wa nchi za magharibi na wanahabari wa Hong Kong walifika mahakamani hapo,lakini hawakuruhusiwa kufuatilia kesi hiyo.
Mahakama hiyo ilisema imesikiliza maoni ya waendesha mashitaka na watuhumiwa, bila kufichua taarifa zaidi za kesi hiyo.
Kabla ya kikao cha kwanza cha kusikiliza kesi hiyo, ubalozi wa Marekani nchini China ulitoa tamko la kutoa wito wa kuachiliwa kwa wanaharakati hao.
Waziri wa mambo ya Nje wa Uingereza Dominic Raab aliitaka China kuendesha kesi hizo kwa haki na uwazi.