NA MWANAJUMA MMANGA

JESHI la polisi Mkoa wa Kusini Unguja linamshikilia Masoud Othman Mzengi (60), mkaazi wa Kidimni kwa tuhuma za mauaji ya mkewe.

Kamanda wa polisi Mkoani humo, Kamishna Msaidizi, Suleiman Hassan Suleiman, akithibitisha kutokea kwa tukio alimtaja marehemu huyo kuwa ni Maryam Bakari Matoja (50) mkaazi wa Kidimni na tukio hilo limetokea Disemba 24 mwaka huu majira ya saa 11:30 jioni.

Kamanda Suleiman alisema tukio hilo lilitokea Kidimni Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo maiti ya Mariyam imekutikana ndani ya kisima ambapo inadaiwa marehemu alitoweka nyumbani kwake tokea Disemba 23 mwaka huu majira ya saa 11:00 alfajiri.

Alisema baada ya kuonekana mwili huo wa marehemu katika kisima zilifanyika juhudi za uokozi wa kikosi cha uokozi KMKM na alipopatikana alikimbizwa hospitali ya Mnazi Mmoja na kufanyiwa uchunguzi.

Kamanda Suleiman alisema chanzo cha tukio hilo katika uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu na mumewe walikuwa na ugomvi baada ya marehemu kutuhumiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwengine.

“Hadi sasa mume wa marehemu huyo aitwae Masoud Othman Mzengi yuko chini ya ulinzi wa polisi kwa ajili ya uchunguzi na mahojiano zaidi,” alieleza kamanda Suleiman.

Hivyo aliwataka wananchi hasa wanandoa kama wamehitilafiana pande hizo mbili kutafuta watu wazima kwa ajili ya kusuluhishwa na badala yake kutochukua uamuzi mikononi mwao.