NA MARYAM HASSAN

MBUNGE wa jimbo la Kwahani, Ahmada Yahya Abdulwakil, ameshiriki katika ujenzi wa tawi jipya la CCM Sebleni kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa ilani ya chama kwa hatua za awali.

Akizungumza katika ujenzi huo, alisema hatua hiyo ni moja kati ya ahadi zake wakati wa kampeni ambao utazidi kukiimarisha chama cha Mapinduzi.

Alisema kwa sasa chama kimezingatia kujenga matawi hayo kupitia viongozi wa majimbo yao ili kuwa ya kisasa kwa mujibu ambavyo yataweza kuleta wananchi wengi.

Aidha alisema, kuwa ujenzi huo umeshirikisha wanaCCM wa jimbo hilo pamoja na viongozi wa wilaya ambao umepata baraka zote.

“CCM ni chama kikubwa chenye kwenda na wakati, na jengo hili litakuwa linakidhi mahitaji yote kwa sababu mfumo uliokuwepo hivi sasa unaendana na tawi lenyewe.” alisema.

Alifahamisha kuwa jengo hilo hadi kumalizika kwake litagharimu shilingi milioni 100 ambapo litakuwa na Ofisi ndogo ya Mbunge na Mwakilishi, ofisi za jumuiya zote za chama, sehemu ya kusomea kwa watoto wadogo ,kusoma chekechea pamoja na ukumbi mkubwa wa mikutano mbalimbali.

Naye mwakilishi wa jimbo hilo, Yahya Rashid Abdallah (Mamba) aliwaomba wanachama wa jimbo hilo kushiriki katika ujenzi huo kwa kutoa nguvu zao ili kuhakikisha ujenzi huo unamalizika kwa wakati.

Katibu wa CCM jimbo la Kwahani, Abdul-rahman Omar Kasongo, alisema kuwa kumalizika kwa ujenzi huo kutasaidia kufanyika vikao vya ndani ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili viongozi wa matawi.

Aidha alisema kuwa kumalizika kwake wanaCCM wengi watanufaika kwa kiasi kikubwa kwani sasa ni siasa na uchumi, hivyo ni lazima kuhakikisha kuwa ukumbi utakaokuwepo hapo utatumika kwa vikao mbalimbali kwa ajili ya shughuli za kijamii na za chama.

Nao wanachama wa jimbo hilo, tawi la Sebleni, walipongeza hatua ya viongozi hao kutekeleza kwa vitendo ahadi walizozitoa kwa wananchi jambo linalowajengea ujasiri katika kushirikiana na viongozi kwa maendeleo ya jimbo lao.