NA AMEIR KHALID

MBUNGE wa jimbo la Chwaka, Haji Makame Mlenge, amesema atahakikisha anashirikiana na wanaushirika wa Hakuweki kulitafutia ufumbuzi tatizo la nguvu ndogo ya maji katika shamba lao.

Akizungumza na wana ushirika hao wakati wa zoezi maalum la kupanda miche ya mitungule kuzindua msimu mwengine wa kilimo hicho huko Uroa.

Alisema ari na bidii walionayo wana ushirika hao ya kujishuhulisha na kilimo, atahakikisha anawaunga mkono kwa kuanza kulitafutia ufumbuzi tatizo la maji katika shamba  hilo ili kilimo chao kilete tija zaidi.

Alisema wanaushirika hao wameitikia wito wa serikali wa kujiajiri wenyewe, hivyo wanapashwa kuungwa mkono katika kuhakikisha wanalima kilimo  cha kisasa ambacho kitawaletea tija wao na familia zao.

‘’Tayari nimesikia tatizo lao kubwa ambalo ni maji wanayo mwagilia katika vipando vyao hayana nguvu ya kupanda katika matangi ya kuhifadhia, hivyo nitahakikisha naanza na hilo, ili kuona linatatuka na muweze kumwagilia maji bila ya shida yoyote na kuvuna mazao mengi’’alisema.

Aidha mbunge huyo aliwataka wanakikundi hao kuwa na tabia ya kuweka hakiba kwa kufungua akaunti ya benki, ili iwasaidiye siku za  baadaye katika maisha yao.

Nao wana ushirika hao walimuelezea mbuge huyo juu ya tatizo la maji ambalo linawasumbua baada ya minara yao ya kuwekea matangi ya kuhifadhia maji kuwa mifupi na kushindwa kumwaga maji kama inavayotakiwa.

Hivyo walimuomba Mbunge huyo kuwasaidia ujenzi ya minara mingine ya kuwekea matangi, ili kuondosha tatizo hilo ambalo linawasumbua kwa muda mrefu sasa na kuwafanya kushindwa kupata ufanisi wa kilimo chao.

‘’Visima tunavyo na vina maji ya kutosha, pampu za kusukumia maji  pia zipo, tatizo letu kubwa ni minara tuliojenga ya kuweka matangi  ya maji ni mifupi sana, hivyo tumemuomba mbunge wetu atusaidiye na tunashukuru amekubali’’alisema.

Ushirika huo, hadi sasa una wanachama 28 wanawake na wanaume na kilimo chao kikubwa ni tungule na pilipili boga ambapo wanalima kwa mfumo wa kumwagilia maji.