NA HAFSA GOLO

MBUNGE wa Jimbo la Fuoni, Abasi Ali Mwinyi amekabidhi kisima cha maji safi na salama kwa wananchi  wa Fuoni  Birikani ikiwa ni utekelezaji wa ilani na ni miongoni mwa ahadi alizoahidi wakati akiwania nafasi hiyo kupitia chama Cha Mapinnduzi.

Abasi wakati akikabidhi kisima hicho katika shehia ya Birikana alisema lengo la ujenzi wa kisima hicho ni kumaliza tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wanaoishi makaazi hayo na maeneo mengine jirani.

Alisema ujenzi wa kisima katika eneo hilo utasaidia kupunguza masafa marefu waliokuwa wakitumia wananchi katika kufatilia huduma hiyo, jambo ambalo limekuwa likichangia usumbufu.

Aidha Abasi aliahidi  kuendelea kutatuzi changamoto hiyo kwa wananchi wa shehia Fuoni Migombani na Kitongani katika kipindi kifupi kijacho ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa ahadi na utatuzi wa kero zinazowakabili wananchi.

Mbali na hilo, alisema Mbunge huyo amejipanga kumaliza tatizo la maji, bali  amedhamiria kuondosha changamoto nyengine za mahitaji ya kijamii yanayowakabili wananchi jimboni humo.

Akizungumzia kuhusu huduma ya  umeme katika visima vitakavyojengwa jimboni humo alisema wananchi watalazimika kuchangia sambamba na kuhakikisha wanavilinda na kuvitunza kwa maslahi yao binafsi.

Mmoja wa wakaazi wa eneo hilo, Maryam Mateo, aliushukuru uongozi wa jimbo hilo kwa utekelezaji wa ahadi kwa wakati sambamba na kumaliza shida ya upatikanaji wa maji safi na salama.

“Tulikuwa tumeota vipara kwa kusaka maji masafa marefu na wakati mwengine inatulazimu kutofanya mambo mengine ya msingi”,alisema.

Alisema ujio wa kisima hicho utasaidia kuondosha kero kwa kinamama na kuweza kufanya shughuli nyengine muhimu kwa wakati ikiwa ni pamoja na uuzaji biashara.

Kwa upande wa Injinia wa Taasisi Human Relief Foundation, Salum Nassor Mohamed,  alisema tatizo lililochangia la ukosefu wa maji safi na salama katika eneo hilo ni kutokana na miundombinu chakafu, hivyo si rahisi kupatikana kwa huduma hiyo kwa ufanisi.