NA SAUDA S. KHAMIS (WNAKUU)

MWAKILISHI wa Jimbo la Bububu ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji,  Mudrik Ramadhan Soraga, amewataka wananchi wa shehia za Mbuzini na  Mkanyageni kuwaelimisha vijana madhara ya udhalilishaji wa kijinsia  katika mzingira wanayoishi.

Aliyasema   hayo huko katika uwanja wa mpira wa Mkanyageni wakati akizungumza na wananchi wa shehia hizo ,kuhusu mapambano ya  masuala ya udhalilishaji wa kijinsia  .

Alisema  wazazi wanajukumu kubwa la kuwalinda watoto kwa kuwaelezea hali ilivyo , kwani wao wanaangalia malezi  wanayowapatia katika maisha yao na familia zao, ili kuweza kujikinga kwa kufanyiwa ukatili huo.

Nae,  Mbunge wa Jimbo hilo, Mwantakaje Haji,  amewataka wananchi hao kutoa ushirikiano pindi yanapotokea matatizo hayo na yuko tayari kushirikiana nao  na kuliondosha kabisa suala hilo katika shehia zao.

Aliwataka  wazazi kujitahidi kulea katika maadili yanayokubalika katika mila na desturi  za kizanzibari na wasiwe woga kutoa ushahidi .

Nao,  wananchi wa shehia hizo, walisema wamechoshwa na mwenendo  wa kesi  kwa muda mrefu mahakamani na  baa za mitaani, kwani  wanapowasilisha matatizo hayo hakuna kinachofanyika na wanashindwa kwenda mbele katika shughuli zao za maendeleo kwa ufuatiliaji  usio mafanikio.

Mkutano  huo ni miongoni mwa mikutano inayoendelea kufanywa na wizara ya afya jinsia na watoto inayokutana na wananchi juu ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.