MADRID, Hispania
NAHODHA wa Barcelona, Lionel Messi, amesema, anatarajia siku moja kucheza soka nchini Marekani, lakini, hana uhakika juu ya hatma yake wakati mkataba wake utakapomalizika mnamo Juni.
Raia huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 33, anaweza kuanza mazungumzo na klabu za nje ya Hispania Januari mwakani.
Uvumi kuhusu maisha yake ya soka ya baadaye umekuwa mkali tangu alipowasilisha ombi la uhamisho mnamo Agosti mwaka huu, baada ya kuonekana yeye ni chanzo cha migongano Nou Camp.
Messi alikiambia kituo kimoja cha televisheni cha Hispania kuwa anasubiri hadi msimu umalizike, na anafikiria kwenda Marekani, lakini, pia angelipenda baadaye arejee Barcelona katika nafasi fulani.
Kwa sasa Barcelona ambayo haikushinda taji lolote msimu uliopita, ipo katika nafasi ya tano katika Ligi Kuu ya Hispania baada ya kuanza vibaya kampeni ya ligi.
(Goal).