MADRID, Hispani

MSHAMBULIAJI wa Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi, amesema jaribio lake la kutaka kuondoka klabuni hapo ambalo liligonga mwamba katika dirisha la uhamisho lililopita liliathiri sana mchezo wake msimu huu.

 Mwezi Agosti mwaka huu mshambuliaji huyo nyota wa Argentina alisema anataka kutumia kifungu cha sheria katika mkataba wake ambacho kingemwezesha kuondoka katika klabu hiyo.

Lakini Barcelona ilikataa, ikisema malipo ya ada ya Euro milioni 700 (£624m) lazima yaafikiwe.

“Nilivuta kila kitu hadi mwanzo wa msimu,” Messi, 33, alikiambia kituo cha televisheni cha Hispania cha La Sexta, “ukweli ni kwamba sasa sina neno, lakini dirisha la uhamisho lililopita lilikuwa ni wakati mbaya sana.”

Messi alifikia rekodi ya mchezaji mkongwe wa Brazil, Pele, ya kufunga magoli 643 ndani ya klabu kwa kuisawazishia Barcelona bao lililoiwezesha kutoka sare dhidi ya Valencia siku ya Jumamosi. Lilikuwa bao la tisa katika mechi 17 za Barcelona, ambao wako nafasi ya tano katika La Liga.

Messi, ambaye anaweza kuondoka Barcelona bila malipo mkataba wake utakapokamilika mwisho wa msimu huu, anaweza kujadiliana na klabu nyingine kuanzia Januari mosi.

Rais wa mpito wa Barcelona Carlos Tusquets, ambaye alichukua nafasi ya uongozi wa klabu hiyo hadi uchaguzi utakapofanywa mwezi Januari baada ya Josep Maria Bartomeu kujiuzulu Oktoba, amesema “kulingana na tathmini ya kifedha ” Messi angekuwa ameuzwa katika dirisha la uhamisho lililopita.