NA MADINA ISSA

MEYA Mstaafu wa Baraza la Manispaa Mjini, Khatib Abdulrahman Khatib, amelitaka baraza la manispaa hiyo kuwekeza katika maeneo mbali mbali ili kuongeza  mapato ya manispaa.

Aliyasema hayyo alipokuwa akizungumza na madiwani wa wilaya hiyo katika kikao cha kwanza cha baraza la madiwani mjini.

Alisema uwekezaji huo utaongeza wigo wa ukusanyaji mapato.

Aidha alilitaka baraza hilo kusimamia vyema utekelezaji wa kanuni, sheria na miongozo ya serikali katika kutekeleza majukumu yake.

Nao baadhi ya madiwani walisema wapo tayari kushirikiana na viongozi hao ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao vyema.

Diwani viti maalum mjini, Maryam Ali Mussa, alisema, atatekeleza ilani kwa vitendo ili kwenda na kasi ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mapema wajumbe wa baraza hilo walipiga kura ya mkuchagua Mstahiki Meya na Naibu Meya wa baraza hilo ambao wataongoza baraza kwa kipindi cha miaka mitano.

 Waliochaguliwa ni Ali Haji Haji kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa Mjini na Naibu wake ni Khadija Ame Haji.

Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Mjini, Ali Haji Haji, alisema baraza hilo limejipanga kubuni vianzio vipya vya mapato ambavyo vitasaidia kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali.