NA KIJA ELIAS, MOSHI

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira,  amepiga marufuku watumishi wa serikali kwenda likizo za mwisho wa mwaka na badala yake wametakiwa kusimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa ya sekondari hususani ya kidato cha kwanza kwenye maeneo yao.

Dk. Mghwira,  alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza Januari 2021, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu huyo wa mkoa.

Dk. Mghwira, aliwataka viongozi wa wilaya, halmashauri na wadau wa maeneo yao kushirikiana kwa karibu na wadau kuongeza vyumba hivyo kabla ya Januari, ili watoto wote waliofaulu waweze kupata nafasi za masomo ya sekondari.

“Baadhi ya halmashauri zina upungufu wa vyumba vya madarasa  hivyo  ninawaagiza  watumishi kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo, ili kila mwanafunzi aliyefaulu apate nafasi ya kidato cha kwanza Januari 2021,  katika kutekeleza agizo hilo likizo za mwisho wa mwaka zimesitishwa,”alisema Dk. Mghwira.