CAIRO,MISRI

SERIKALI ya Misri imetangaza kuwa,karibuni itafungua tena ubalozi wake katika nchi jirani ya Libya.

Mohammed al Qablawi Msemaji wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya alithibitisha habari hiyo baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa Misri uliotembelea Libya na kuongeza kuwa, Cairo iliahidi kwamba karibuni ubalozi wa Misri utafunguliwa mjini Tripoli.

Akihojiwa na mtandao wa habari wa Arabi 21, Mohammed al Qablawi alisema, lengo la ziara ya ujumbe huo wa Misri nchini Libya ni kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili.

Jumapili ya wiki iliyopita, ujumbe mmoja wa ngazi za juu wa Misri ulitembelea Libya  ikiwa ni mara kwa kwanza tangu mwaka 2014  na kuonana na viongozi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya.

Itakumbukwa kuwa, katika vita vya ndani vya Libya, muda wote huu Misri ilikuwa ikimuunga mkono jenerali muasi Khalifa Haftar aliyekuwa anaendesha vita vya kuipindua Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayotambuliwa rasmi kimataifa.

Tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni za kumpindua kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi hadi hivi sasa, nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika haijawahi kuwa na utulivu na hivi sasa kuna serikali mbili zinazotawala nchini humo.

Mbali na Misri, jenerali muasi Khalifa Haftar anaungwa mkono pia na nchi kama Saudi Arabia, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi ikiwemo Ufaransa.