NA MOHAMED HAKIM

JAMII imetakiwa kushirikiana na serikali katika kuutunza na kuuimarisha Mji Mkongwe ambao ni miongoni mwa vivutio vya utalii, ili kuunga mkono kasi ya Rais ya kukuza uchumi kupitia sekta hiyo.

Ofisa Mtendaji wa jumuia ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe (ZSTHS) Makame Juma, aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili huko ofisini kwake Forodhani mjini Unguja.

Alisema ili kuweka haiba nzuri ya mji mkongwe, jamii inapaswa kuunga mkono juhudi za serikali katika kujua thamani ya mji huo, jambo ambalo litawapelekea kuutunza kwa kuweka mazingira safi na salama muda wote.

“Malengo ya Rais katika kuikuza sekta ya utalii yanaonekana wazi, kwani Serikali ya awamu ya nane kwa kulipa umuhimu suala zima la utalii imeunda Wizara ya Utalii na mambo ya kale inayojitegemea, hivyo mbali na wadau mbali mbali kuunga mkono suala hili, wananchi wanapaswa kutoa mashirikiano yao ili kwa pamoja kuukuza uchumi wa nchi”

Aidha alisema, jumuia yao ina mikakati mbali mbali ya kuhakikisha wanaweka safi na kutunza maeneo ya mji mkongwe ambao ni urithi unaowavutia wageni na kupelekea kukua kwa uchumi wa nchi.

Akiitaja miongoni mwa mikakati ambayo wapo njiani kuitekeleza endapo tu watapata ufadhili, ni kuweka madebe ya taka katika maeneo yote ya mji mkongwe ili kuhakikisha hali ya usafi na unadhifu katika mji huo.

Sambamba na hilo alisema, jumuia yao imeanza kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala zima la umuhimu wa kuutunza na kuimarisha Mji Mkongwe ambao ni uruthi na kivutio cha wageni.