MOHAMED Bouazizi alikuwa kijana maarufu aliyekuwa akiuza bidhaa za matunda na mboga mitaani ya mji wa Sidi Bouzid uliopo nchini Tunisia kwa maana nyengine hujakosea ukimuita mmachinga.

Mboga na matunda aliyokuwa akiuuza katika mitaa mbalimbali ya mji huo, alikuwa akirandisha kwa kutumia mkokoteni kwa ajili ya kuwafikishia huduma wateja wake katika mji huo.

Kumbukumbu zinaonesha alizaliwa Machi 29 mwaka 1984 katika mji wa Sidi Bouzid, hata hivyo kifo chake kilichotokea Disemba 17 mwaka 2010 sio tu kisababisha simanzi kubwa, lakini pia kimeleta mabadiliko kwenye siasa za baadhi ya nchi za kiarabu.

Tunaweza kusema kuwa kifo cha Mohamed Bouazizi ndicho kilicholeta mageuzi makubwa katika kadhaa za kiatabu huku tukishuhudia baadhi ya viongozi waliodumu kwa muda mrefu kuondolewa madarakani kwa kile kilichofahamika kama ‘Arab Spring’.

‘Arab Spring’ ilianzia nchini Tunisia kutokana na kifo cha Mohamed Bouazizi, ambapo ilikuwa Disemba 17 mwaka 2010, kijana huyu alikumbana na nguvu ya dola kwa kufanya biashara bila kibali ambapo alinyang’anywa mkokoteni na kibaya zaidi alipigwa kibao na askari polisi wa kike kitendo kilichomuumiza sana.

Baada ya kutendewa vivyo sivyo, kijana huyu aliamua kwenda katika ofisi za gavana wa jimbo kulalamika ila kwa bahati mbaya hakuruhusiwa kuonana na gavana jambo liliomuongezea hasira na machungu.

Kutokana na hasira alizokuwa nazo, kijana huyu aliamua kwenda sheli na kununua petroli katika kidumu na kurudi mbele ya jengo la ofisi ya gavana ambapo aliamua kujimwagia petroli hiyo na kisha kujitia kiberti na kuungua vibaya.

Alikimbizwa hospitali akiwa na majeraha makubwa ya moto ambapo alilazwa kwa zaidi ya wiki mbili akipatiwa matibabu ya kujaribu kuokoa maisha yake, hata hivyo ilipofika Januari 4 mwaka 2011, Bouazizi aliaga dunia.

Kitendo cha Bouazizi kujilipua ndio kilichoamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuanza maandamano ya kupinga utawala wa raisi wa wakati huo, Zinel al-Albidine Ben Ali.

Mohamed Bouazizi kijana shujaa ambaye historia ya Afrika haiezi kumueka kando, hakuwa msomi wa elimu ya juu baada ya baba yake mzazi kufariki akiwa na umri wa miaka mitatu, na kisha mama yake mzazi kuolewa na mume mwingine fukara.

Bouazizi alizaliwa katika mji wa Sidi Bouzid, uliopo umbali wa kilomita 300 kutoka jiji la Tunis, maisha yake yote yalikua katika mji wa Sidi Bouzid kuanzia kuzaliwa na kupata elimu ya msingi.

Baada ya kufikisha umri wa kuanza kujituma alifanya majaribio kadhaa ya kuomba kazi na hakufanikiwa kutokana na elimu yake kutokua kubwa na pia kukosa mtandao wa watu wa kumsaidia kupata ajira.

Kwa mujibu wa mama yake mzazi aliwahi pia kuomba kujiunga na jeshi la Tunisia hata hivyo alikosa nafasi na baada ya hayo yote mwaka 2002 aliamua kufanya kazi za vibarua na kujikusanyia mtaji ambao ulimwezesha kufungua genge la kuuza matunda mwaka 2003.

Kazi hiyo ya kujiajiri ndiyo iliyokuwa ikiilisha familia yake iliyokua na watu wananena kazi hiyo aliendelea nayo kwa mafanikio makubwa ya kujipatia kipato kilichoendesha maisha ya familia yake katika kumudu mahitaji muhimu.

Watu wa kawaida katika mitaa aliyozoea kufanya bishara yake walimpenda sana na inasemekana alikua na hulka ya kutoa matunda bure kwa baadhi ya familia maskini na hilo lilimfanya kuwa maarufu.

Mnamo Disemba 17 mwaka 2010 majira ya asubuhi alikutana na ofisa wa manispaa wa kike aitwaye Faida Hamdi na kumtaka Bouazizi aonyeshe leseni ya biashara.

Bouazizi hakuwa na leseni na mara zote polisi au maofisa wa serikali walipokuwa wakihitaji leseni na yeye kutokua nayo alikua anatozwa faini kiasi cha dinari 10 ambazo ni sawa na dola 7 za marekani fedha ambazo zilikuwa sawa na faida yake ya kazi ya siku moja.

Faida Hamdi alikataa kupokea faini na badala yake alimtukana marehemu baba yake Mohamed Bouazizi na pia kumtandika kibao, tukio hilo lilileta mtafaruku na Faida Hamdi aliwaita askari na wao walipokuja walimpiga Mohamed Bouazizi na kuchukua matunda yake yote na kuondoka nayo.

Hiyo ilikua kama saa nne asubuhi siku hiyo ya Disemba 17 mwaka 2010. Kutokana na hali hiyo Mohamed Bouazizi aliona kuwa kwa lililotokea busara ni kwenda ofisi za manispaa ya Sidi Bouzid na kulalamikia kitendo kile cha kuchukuliwa matunda yake yote katika genge lake.

Alipofika watumishi wa manispaa walimpuuza na hakuna aliyekua tayari kumsikiliz, kitendo hicho kilimlazimu Mohamed Bouazizi kuondoka katika ofisi hizo.

Alikwenda hadi katika kituo cha mafuta na kununua vimiminika hivyo na badae kiberiti. Mohamed Bouazizi hakumshirikisha yeyote katika uamuzi huo.

Baada ya hapo alirejea katika ofisi za manispaa na kujilipua yeye mwenyewe kwa lengo la kutoa somo kwa wanyanyasaji, hiyo ilikua saa tano na nusu asubuhi baada ya kujilipua alikimbizwa hospital na taarifa za tukio hilo.

Lilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii ya facebook na you tube na watu nchini Tunisia walikasirika sana na kwa kumuunga mkono Mohamed Bouazizi waliamua kuanzisha maandamano ya amani na ya mfululizo nchi nzima.

Muitikio wa maandamano ulikua mkubwa mjini na vijijini na hadi kufikia tarehe 28 Disemba mwaka 2010 maandamano yalishamiri na kumlazimu rais wa wakati huo wa Tunisua Zine El Abidine Ben Ali kumtembelea Mohamed Bouazizi hospitali alipokuwa amelazwa.

Mnamo disemba 28 mwaka 2010, serikali ilitangaza kumgharamikia Mohamed Bluazizi katika matibabu yake yote katika hospital iliyokua karibu na jiji la Tunis.

Rais Ben Ali ambaye kwa wakati huo alikua madarakani kwa miaka 23 aliona maandamano yamekolea ya kumtaka ang’oke madarakani na hivyo kuagiza police kudhibiti waandamanaji pamoja na kufanya mabadiliko kadhaa katika baraza lake la mawaziri.

Wakati hayo yakiendelea rais Ben Ali alitangaza kuwa serikali itatoa ajira 3,000 na kwamba ataitisha uchaguzi ndani ya miezi sita na kwamba hatabadili kwa maana hiyo ukomo wake wa urais ungekua 2014.

Waandamanaji walipokea ahadi hizo ila hakuna aliyeziamini wala kuzitumia kama kichocheo cha kutoendelea na maandamano na ilipofika siku ya Jumanne ya Januari 4, Mohamed Bouazizi alifariki na kusababisha maandano kudumu bila kujali hatima ya waandamanaji.

Pamoja na serikali kusema kuwa waandamanaji ni magaidi, wananchi walipuuza kauli hizo na hiyo ilienda hadi siku ya Ijumaa ya Januari 14 mwaka 2011 ambapo rais Ben Ali alitangaza kujiuzulu na kukimbilia uhamishoni Saudi Arabia.

‘Arab Spring’ pia ilizikumba nchi za Misri ambapo wananchi nchini humo walimuondoa Hosni Mubarak, Libya Muammar Gaddafi na Abdullah Saleh wa Yemen naye aliondolea madarakani.

Gaddafi aliuawa mwaka 2011 katika vita vya ndani vya Libya, Abdullah Saleh aliuawa mwaka 2018 katika mlipuko wa bomu na Bin Ali ameaga dunia Septemba mwaka huu wa 2019 nchini Saudi Arabia kutokana na maradhi.