RABAT,MOROCCO

MAANDAMANO yanaendelea nchini Morocco ya kupinga hatua ya watawala wa nchi hiyo ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel ambao mikono yake imejaa damu za watu wasio na hatia wa ndani na nje ya Palestina.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, wananchi wa mji wa Tangier waliendeleza maandamano ya kuupinga utawala wa Israel na kulaani hatua ya watawala wa nchi hiyo ya kutangaza uhusiano wa kawaida na wafanya jinai hao.

Katika maandamano hayo, mbali na kubeba mabango ya kila namna,waandamanaji walisikika wakisema kwa sauti kubwa kwamba Palestina ni amana kwao.

Kwa upande wao,watumiaji wa mitandao ya kijamii walisambaza picha mbali mbali za kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na kulaani uamuzi wa Morocco wa kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel.

Upinzani dhidi ya kitendo cha baadhi ya nchi za Kiarabu cha kujidhalilisha kwa Waisrael na kutangaza uhusiano wao wa kawaida, kinaendelea kulaaniwa kote ulimwenguni.

Hatua ya karibuni kabisa ni ya Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti ambaye alisema kuwa, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel ni jambo lisilokubalika kwani kufanya hivyo ni kinyume na mpango wa amani wa Kiarabu.

Mbali na Morocco, nchi nyengine za Kiarabu ambazo zilianzisha uhusiano na Israel hivi karibuni ni pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain na Sudan ambazo zilianzisha uhusiano na utawala huo dhalimu katika fremu ya njama za Marekani,za kudhoofisha uungaji mkono wa nchi za Kiarabu kwa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina.