NA MWANDISHI WETU
ZAIDI ya wakulima 21,000 kutoka maeneo mbali mbali Unguja na Pemba, wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kukuza kilimo cha mboga,matunda na viungo (Viungo Project) katika shehia zaidi ya 50 Unguja na Pemba.
Hayo yalilezwa na Meneja Utafiti na Ufuatiliaji wa mradi huo, Ali Mbarouk, wakati akizungumza na maofisa wa mabaraza ya miji katika ukumbi wa baraza la magharibi ‘B’ Unguja.
Alisema mradi huo wa miaka minne unaotekelezwa na TAMWA-Zanzibar, jumuiya ya kuhifadhi misitu asili Pemba (CFP) na taasisi inayojihusisha maendeleo ya watu kutoka Dar es Salam (PDF) unalenga kuhamaisisha kilimo bora kwa maslahi ya wote.
Alisema mradi huo utatekelezwa katika wilaya tisa tano kutoka Unguja na nne za Pemba ambapo maeneo yote yamezingatia ushauri wa watalamu wa wizara ya kilimo.
Alisema miongoni mwa malengo ya mradi huo ni kuwaleta karibu wadau wanaohusika na uzalishaji wa mazao na kuongeza ubora wa uzalishaji wa bidhaa za kilimo, kuongeza lishe na uhakika wa chakula kwa wakulima.
Sambamba na hayo alisema mradi huo utaongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa, kuboresha masoko ya nje na ndani kwa sababu imebainika kwa miaka mingi bidhaa za Zanzibar zimeshindwa kufanya vizuri katika masoko ya nje.
Alitaja mikakati ya kufanikisha mradi huo kuwa ni pamoja na kutoa elimu ya kilimo bora kisichotumia mbolea zenye madhara kwa walaji.
Alisema tayari kupitia washirika katika mradi huo taasisi ya kimataifa inayojihusisha na uhifadhi wa misitu (CFI) ya Canada, wamekusudia kukuza soko la bidhaa za Zanzibar katika mataifa ya kigeni.
Alisema anaamini kuanza kwa mradi huo kutafunga fursa zaidi na kuinua uchumi kwa wananchi.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, walisema mradi huo umekuja wakati muafaka ambapo wananchi wengi wanahitaji maedeleo.
Nahla Abdulhalim Mhamed, Ofisa masuala mtambuka kutoka baraza la mji wilaya ya kaskazini ‘B’, alisema ujio wa mradi huo utakua mkombozi kwa wakulima.
Makame Kitwana Makame, Msaidizi Mkurugenzi kilimo, maliasili na mazingira Wilaya ya Kati, alisema mradi huo iwapo utatekelezwa vyema utaleta manufa.
Mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa shirika la CFI.