ADDIS ABABA,ETHIOPIA

WATU watatu wameuawa na wengine watano wamejeruhiwa baada ya bomu lililotelekezwa kuripuka katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Mripuko huo ulitokea Jumapili katika eneo la Lideta lililoko viungani wa Addis Ababa.

Kamanda wa Polisi katika eneo hilo, Alemayehu Ayalke aliliambia shirika la habari la serikali la EBC kuwa, waliouawa katika mripuko huo wa bomu ni watu wasio na makaazi na wanaoshi mitaani.

Hakuna kitu chochote kinachoashiria kuwa mripuko huo una muungano na mgogoro unaoendelea kushuhudiwa katika eneo la Tigray, kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Serikali ilisema uchunguzi wa kubaini chanzo cha mripuko huo umeanza na kwamba wananchi watapatiwa taarifa ya kina kuhusu mkasa huo pale uchunguzi utakapomalizika.

Eneo la Tigray lililoko kaskazini ya Ethiopia limeshuhudia mapigano katika wiki za karibuni kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray (TPLF).

Serikali ya Addis Ababa, ambayo inaituhumu TPLF kuwa inataka kulitenganisha eneo la Tigray na ardhi ya Ethiopia, ilitangaza hivi karibuni kuwa vikosi vya jeshi viliudhibiti mji wa Mek’ele, ambao ni makao makuu ya eneo hilo.

Mapigano hayo yalisababisha watu 50,000 wakimbilie katika nchi jirani ya Sudan.