NA MARYAM HASSAN

MTOTO wa miaka 17 mkaazi wa Mitakawani wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja, amepandishwa mahakamani kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenzake wa kike mweye umri wa miaka 14

Akiwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Khamis Ali Simai na kusomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka, Sara Omar Hafidh, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Mtoto huyo alidaiwa kutenda kosa hilo mnamo Novemba 25, 2018 majira ya saa 2:00 usiku, huko Mitakawani wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Inadaiwa kuwa, siku hiyo alidaiwa kumuingilia kimwili mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 (jina tunalo) ambaye si mke wake, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mara baada ya kusomwa shitaka lake hilo mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana, jambo ambalo lilikubaliwa kwa sababu ni mtoto anayelindwa na sheria.

Wakili huyo alisema, kwa kuwa mshitakiwa ni mtoto apewe masharti madhubuti ambayo yatatekelezeka pamoja na kuwa na wadhamini madhubuti watakaohakikisha anapatikana kila kesi hiyo inapofikishwa mahakamani.

Hivyo kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Februari 18 mwakani, huku upande wa mashitaka ukitakiwa kuwasilisha Afisa Ustawi wa Jamii, kwa sababu kama hatokuwepo Asifa huyo kesi hiyo haitoweza kusikilizwa.

Baada ya maelezo hayo, mshitakiwa huyo alitakuwa kusaini bondi ya shilingi 500,000 na wadhamini watakaosaini kima hicho hicho, pamoja na barua ya Sheha na kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi jambo ambalo amelitimiza.