NA KIJA ELIAS, HAI

MKAZI wa Kijiji cha Muroma Kata ya Masama Kati, wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro aliyefahamika kwa jina la Welanzari Kimaro (56) ameuawa kwa kukata katwa na panga kichwani na kisogoni na mwanawe wa kumzaa kisha muuaji huyo kutoweka kusikojulikana.

Aidha muuaji huyo, aliyefahamika kwa jina la James Wenzari Kimario mwenye umri wa miaka (24) kabla hajatoweka kusikojulikana alimjeruhi pia Mama yake mzazi  aliyekuwa jikoni akiandaa kifungua kinywa kwa ajili ya familia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashuhuda wa tukio hilo walisema muuaji anayefahamika kwa jina la James Welanzari Kimario, alitekeleza azma yake mnamo Desemba 17, mwaka huu mapema asubuhi wakati baba yake akifanya usafi wa nje ya nyumba.

“Siku ya tukio baba yake aliamka asubuhi akawa anakatakata fensi ya miti iliyopo nyumbani hapo na mkewe alikuwa akiandaa chai kwa ajili ya kifungua kinywa,” alisema shuhuda ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Walisema baada ya baba yake kumaliza kazi ya kukata kata fensi aliingia ndani kwa ajili ya kupata kifungua kinywa baada ya kutengewea na mke wake, kijana huyo alifika na kuingia ndani bila kuuliza chochote na kuanza kumkata kata baba yake kwa panga.

“Baada ya kuona tukio hilo mama yake alipiga kelele za kuomba msaada, kija huyo aliachana na baba yake na kwenda kumkatamkata mama yake kwa panga na baada ya kuona kuwa ameua kijana huyo alikimbia kusikojulikana,”walisema mashuhuda

Mashuhuda hao waliongeza kuwa marehemu ambaye alikuwa mkulima hakuwa na ugomvi na mtoto wake huyo, ambaye alikuwa akiishi nyumbani kwa shangazi yake umbali mfupi kutoka ilipo nyumba ya baba yake.

“Kijana aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa anakaa nyumba ya pili ya shangazi yake ambapo sio mbali sana na nyumba ya baba yake mzazi, na hatukuwahi kusikia ugomvi baina yao na mpaka sasa hatujui ni mazingira gani yalimpelekea kijana  huyo kuchukua uamuzi wa kumuua baba yake,” alisema shuhuda mwingine.