NA ASYA HASSAN

MWAKILISHI wa Jimbo la Malindi, Mohammed Ahmada Salum amewataka wanafunzi waliomaliza kidato cha nne skuli ya Forodhani wasibweteke na badala yake kuendeleza kusoma ili waweze kufikiwa kwa lengo la serikali la kuanzishwa kwa uchumi wa buluu hapa nchini. 

Mwakilishi huyo alisema hayo katika skuli ya Forodhani alipokuwa katika mahafali ya kidato cha nne cha wanafunzi wa skuli hiyo, ambapo alisema serikali imekuwa ikisisitiza kuimarishwa kwa uchumi wa buluu hatua ambayo haiwezi kufanikiwa bila ya kuwepo wataalamu.

Alisema nchi nyingi duniani zimepiga hatua kubwa ya maendeleo baada ya kuwa na wasomi wengi na wataalamu wa fani mbalimbali ambao wametoa michango katika kufanikisha maendeleo hayo. 

Hata hivyo alifahamisha kwamba lengo la Zanzibar ni kuelekea kwenye uchumi wa juu, lakini ili kufikia hatua hiyo lazima nchi iwe na wasomi na wataalamu wa kutosha katika fani mbalimbali watakaoweza kusimamia na kubuni maendeleo.

Sambamba na hayo Mwakilishi huyo aliwasisitiza wanafunzi hao kujali na kuthamini juhudi za serikali katika kuipigania sekta hiyo kwa lengo la kuweza kufanikisha upatikanaji wa maendeleo ya nchi.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi na wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada za serikali katika kuimarisha sekta ya elimu ili iweze kupiga hatua zaidi ya maendeleo.

Mbali na hayo aliwasisitiza walimu, wazazi na wanafunzi wa skuli hiyo kuwa na mashirikiano ya pamoja kwani kufanya hivyo ni chachu kuwafanya wanafunzi kupiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia masomo yao.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa skuli hiyo Mwanajuma Maalim Khamis, alitumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi hao kutotosheka na elimu hiyo na badala yake kuendelea kujisomea kupitia fani tofauti ili iwasaidie katika maisha yao na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia changamoto zilizopo ndani ya skuli hiyo mwalimu huyo alisema ni pamoja na upungufu wa kompyuta za kusomea hali ambayo inasababisha wanafunzi hao kushindwa kufanya vizuri katika masomo hayo na ukizingatia huu ni wakati wa sayansi na teknolojia.