NA KHAMISUU ABDALLAH 

MWANADADA aliyeondosha uaminifu kwa kuchukua shilingi 3,100,000 amepelekwa rumande hadi Disemba 21 mwaka huu, kesi yake itakapofikishwa tena kwa ajili ya kusikilizwa.

Anna John Samuel (25) mkaazi wa Bububu, alipelekwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana aliyopewa mahakamani aliposhitakiwa kwa kosa la wizi baada ya kuaminiwa.

Hakimu wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe Asya Abdalla Ali, alimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 2,000,000 za maandishi na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho za fedha za maandishi na wawe na barua za Sheha wa Shehia wanazoishi na kitambulisho kinachoonesha picha zao.

Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Suleiman Yussuf, kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la wizi baada ya kuaminiwa, kinyume na kifungu cha 251 (1) na 264 (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Anna aliaminiwa na Queen Braiton Moshi kwa kupewa fedha shilingi 3,100,000 kwa lengo la kumkabidhi Law James Sogga, matokeo yake alishindwa kumpatia fedha hizo jambo ambalo ni kosa kisheria.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Disemba 6 mwaka jana majira ya saa 3:00 za asubuhi huko Mbuzini.