NA NASRA MANZI

MWENYEKITI wa  UWT Wilaya Kusini Unguja  AbdulAziz Hamad Ibrahim, amelitaka Baraza la Umoja wa wanawake Tanazania Wilaya hiyo kuendelea kuongoza na kusimamia haki,usawa kwa wanawake ili kujiinua kiuchumi.

Akizungumza  na wajumbe wa UWT katika ufunguzi wa kikao kilichofanyika kwenye  ukumbi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Kusini Mkoa wa kusini Unguja,alisema endapo usimamiaji  wa haki unakuwa imara utasaidia kupatikana maendeleo katika harakati zao za kila siku.

Hata hivyo, alisema mashirikiano ya pamoja yatasaidia kuongeza mbinu za kuwanyanyua kwani wanawake katika umoja huo wamefanya kazi kubwa katika kuiletea maendeleo nchi yao.

“Kinamama mmefanya kazi ya kuhamasisha kwani kazi kubwa mliyoifanya katika uchaguzi Mkuu uliopita yote kutokana na umoja na ushirikiano wenu  kwa ajili ya kukiletea chama mafanikio” alisema.

Aidha alieleza ni vyema kinamama kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali kwa kuiletea Zanzibar mafanikio na kuachana na makundi ambayo hayataleta tija katika utendaji wao wa kazi.

Akizungumzia suala la elimu kwa vijana aliwataka wajumbe hao kufanya jitihada katika ziara zao, ili vijana kujikita na elimu kwa ajili kupatikana ufaulu mzuri katika masomo yao.

Akifunga kikao hicho mjumbe wa kamati ya utekelezaji Baraza la umoja wa wanawake Tanzania Wilaya hiyo,  Rahma Kassim Ali, alisema ni vyema wanawake kuacha muhali wa kutoa ushahidi kwa vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto ili kupatikana taifa bora.

Hivyo aliwapongeza umoja wa wanawake katika  Wilaya hiyo kwa jitihada walizozifanya katika kukiletea ushindi mkubwa chama cha Mapinduzi (CCM) Katibu wa UWT Wilaya hiyo Sihaba Fadhil Pandu alisema ni vyema wajumbe kusimama imara  chama cha Mapinduzi katika majukumu yao ili  chama hicho kuendelea kushinda.