NA MARYAM HASSAN

Hashim Linus Magoho (37) mkaazi wa Nyarugusu, amehukumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka miwili, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la wizi.

Adhabu hiyo imetolewa na Hakimu wa mahakama ya mkoa Mwera Said Hemed Khalfan, baada ya upande wa mashitaka wa serikali kuwasilisha mashahidi wanne ambao walithibisha kosa dhidi ya mshitakiwa huyo.

Hakimu huyo alisema, adhabu kwa mshitakiwa huyo imezingatia hoja za pande zote mbili kwa kuwa mshitakiwa alitenda kosa la wizi baada ya kuaminiwa.

Kabla ya kupewa adhabu hiyo, mshitakiwa aliiomba mahakama kumpa adhabu ya kifungo cha nje na kama haitowezekana basi apigwe faini ili apate kulipa.

Ombi la mshitakiwa huyo halikuzingatiwa mahakamani hapo na badala yake amehukumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka miwili.

Aidha Hakimu Said alisema, katika adhabu hiyo haki ya rufaa imetolewa kwa upande uliokuwa haujaridhika na adhabu hiyo.

Kesi hiyo imefunguliwa Febuari19 mwaka huu na kuanza kusikilizwa ushahidi Machi 4 mwaka huu ambapo jumla ya mashahidi wanne walisikilizwa.

Mapema wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ayoub Nassor, alisema hana kumbu kumbu ya makosa ya zamani kwa mshitakiwa huyo.

Hivyo aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili kupunguza vitendo hivyo ndani ya mkoa wa Kusini.

Kosa hilo anadaiwa kutenda Febuari 8 mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni, huko Tunguu wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa huyo kwa nia ya kujimilikisha na bila ya kuwa na dai la haki, aliwaminiwa na Amour Abdalla Amour kwa kukabidhiwa fedha taslimu shilingi 750,000 kwa lengo la kuzipeleka kwa Mariam Suleiman Mbaraka na badala yake alishindwa kuzipeleka hizo wala kuziresha, jambo ambalo ni kosa kisheria.