Na Maryam Hassan
ALIYEKIMBIA mahakama kwa kipindi kirefu, amehukumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita kwa kosa la kuba nazi 13.
Adhabu hiyo ilitolewa katika mahakama ya wilaya Mwera chini ya Hakimu Rauhia Hassan Bakari Oktoba 1 mwaka huu, bila ya mshitakiwa huyo kuwepo mahakamani.


Mshitakiwa huyo ni Rashid Ali Abdalla (30) mkaazi wa Tunguu, ambae alifikishwa mahakamani tokea Machi 9 mwaka huu kwa kosa la wizi wa mazao.
Mara baada ya kusomwa hukumu ya kesi hiyo ambapo mahakama ilimtia hatiani kwa kuridhika na ushahidi uliotolewa, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Sara Omar Hafidh, anayeisimamia kesi hiyo, aliiambia mahakama kuwa hana kumbukumbu ya makosa ya nyuma juu yake.


Aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria, ili iwe ni fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama hiyo ya wizi wa mazao.
Katika adhabu hiyo, mshitakiwa huyo alitakiwa kulipa faini ya shilingi 6,500 pamoja na fidia ya kiwango kama hicho cha fedha kwa mlalamikaji.
Tukio hilo limetokea Septemba 23 mwaka 2018 saa 1:30 za usiku, huko Tunguu wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.


Mshitakiwa kwa njia ya kudanganya na bila ya kuwa na dai la haki, aliiba nazi 13 ambazo hazijafuliwa zenye thamani ya shilingi 6,500 mali ya Nassor Salum Baeshi, kitendo ambacho ni kosa kishera.
Katika kesi hiyo jumla ya mashahidi wanne walifikishwa mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi dhidi ya mshitakiwa huyo.