NA JOSEPH NGILISHO, MONDULI

MKAZI mmoja wa Kitongoji cha Makuyuni Juu, wilaya Monduli Mkoani Arusha, Ester Mollel (65) ameuawa na Tembo kwa kukanyagwa wakati akiokota kuni akiwa na wenzake.

Tukio hilo, limetokea juzi majira ya saa sita mchana ambapo tembo mmoja aliyekuwa kwenye eneo la malisho alimvamia ghafla mkazi huyo na kuanza kumshambulia kwa pembe na kumkanyaga kanyaga  na kusababisha kifo chake.

Akiongelea tukio hilo Mwenyekiti wa kijiji cha Makuyuni, Ngayok Mollel,  alisema kuwa marehemu kabla ya tukio hilo alikuwa na wenzake wakiokota kuni maeneo hayo, lakini ghafla walisikia mlio wa Tembo na kuanza kukimbia.

Alisema wenzake na marehemu walifanikiwa kukimbia lakini marehemu kutokana na umri wake kuwa mkubwa alishindwa kukimbia ndipo Tembo aliyekuwa akiwakimbiza alipofanikiwa kumpiga pembe na kuanza kumkanyaga kiasi cha kutotambulika.

“Matukio ya wananchi kuuawa ama kujeruhiwa na Tembo yamekuwa yakitokea Mara kwa Mara hapa Makuyuni na hakuna jitihada zozote zinazochukuliwa na mamlaka licha ya taarifa kuzitoa ” Alisema Mwenyekiti 

Aliongeza kuwa Tembo hao wamekuwa wakijivinjari kwenye makazi ya watu wakitoka katika hifadhi za Manyara na Tarangire wakitafuta maji na malisho yasiyo na bughudha.

Naye Mkazi wa Makuyuni, Peter Lesingai, Alisema kuwa matukio ya watu kuuawa ama kujeruhiwa na Tembo yamekuwa kawaida katika kijjji hicho kwani ndani ya wiki hii kijana aitwaye Mjomba Soingei Mollel (24) Mkazi wa Kijiji cha Naitolya, amelazwa katika hospitali ya rufaa KCMC baada ya kujeruhiwa vibaya na Tembo kwa kutobolewa tumbo na pembe.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Salumu Hamduni, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhali ya kuepuka kwenda kwenye maeneo hatarishi yenye wanyama wakali kama Tembo na wengine.